Tuesday, December 13, 2011

Uongozi bila dira

Kwa dira za kuchomoa, na maneno kuambiwa,
Kwa sera za kupakua, kupika wasiojua,
Kwa sera za kusifiwa, na ukweli kutojua,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Ukubwa wenye hadaa, ahadi usiojua,
Kwa baraka za kung'aa, huku nchi inasinyaa,
Hakuna linalokua, hata maua kumea,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Ukubwa wa kutumiwa, wengine kwenda wafaa,
Kwako panapoungua, na sababu hujajua,
Vichaa unapodhania, watu wako wamekua,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Cheo mtu kuchezea, ya wengi akakataa,
Chama anayetetea, nchi akaachilia,
Mustakabali balaa, na hakuna asiyejua,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Taifa la kutanua, wakuu kujinyanyua,
Watu wanadidimia, na nchi inaangamia,
Ibilisi ahofia, hata yeye hatokaa,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Vijiji wasiokweza, nchi hawataiweza,
Ni mkuza kutengeza, majirani ukaiza,
Shamba lazima kumezwa, sangara ikija anza,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Zawaka nguvu za giza, tusubiri miujiza,
Huacha kutuangaza, wakazima kujitunza,
Hujificha kama funza, kwa siri kuangamiza,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

Kazi nimeimaliza, wenye akili kumeza,
Majinuni watabeza, na ubaya kutangaza,
Ila azizi Muweza, ukweli atatujuza,
Uongozi bila dira, nchi haiendi popote!

No comments: