Friday, December 30, 2011

Kuchota maji nchini

Amini usiamini, maji sasa ni muhimu,
Watu waenda kazini, maji kazi ya kudumu,
Yakikosekana ndani, amani haitadumu,
Kuchota maji nchini, sasa kazi ya kudumu!

Na walio mashakani, kinamama wahudumu,
Wanatembea gizani, jamaa kuwakirimu,
Asubuhi na jioni, hii ni yao hukumu,
Kuchota maji nchini, sasa kazi ya kudumu!

Posho wanazisaini, walao aisikirimu,
Kinamama vijijini, hakuna wa kuwarehemu,
Hili lazidi karni, laendelea kudumu,
Kuchota maji nchini, sasa kazi ya kudumu!

Maji yenyewe topeni, kukamua ni muhimu,
Hatukiri wa mjini, vijiji wavidhulumu?
Yakiwa ya kisimani, meupe hayatakua?
Kuchota maji nchini, sasa kazi ya kudumu!

Waruzuku vijijini, sisi tusiowafahamu,
Tuache kuwazaini, tufanze ya kugharimu,
Waipate afueni, nchi wawe nayo hamu,
Kuchota maji nchini, sasa kazi ya kudumu!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: