Friday, December 16, 2011

Siwezi kuwa mtume

BURE mnanisifia, kwa haya ninayoyajua,
Wahyi sijajaliwa, ni yangu nafikiria,
Umbeya sijaletewa, ukweli ninatohoa,
Siwezi kuwa mtume, dini yangu yakataa!

Wa mwisho keshafikia, Aliamini mzawa,
Dhaifu niliyekuwa, iweje mimi kupewa,
Tena ninauhofia, ubora sijatimia,
Siwezi kuwa mtume, uwalii naishia!

Vitabu navitambua, siwezi kuongezea,
Uongo ninahofia, motoni kuja nitia,
Salama naililia, kiyama kikiingia,
Siwezi kuwa mtume, dini yangu yakataa!

Ninailani dunia, ilivyojaa hadaa,
Ibilisi kaingia,na pepo twaidhania,
Kumbe tunaangamia, huku tunaangalia,
Siwezi kuwa mtume, uwalii naishia!

Mitume nawasalimia, nyie mlioteuliwa,
Na heri nawatumia, na mimi kuniombea,
Na siku nikijaliwa, kuja kuwasalimia,
Siwezi kuwa mtume, dini yangu yakataa!

Manabii mlokua, salama nawatakia,
Dini kuiangalia, mmoja inayemjua,
Na pia kuwafichua, uongo wanaotoa,
Siwezi kuwa mtume, uwalii naishia!

No comments: