Sunday, December 25, 2011

Dini ikinunuliwa

Mungu atawahukumu, wote wanaonunuliwa,
Amri wakaisalmu, kafiri kutumikia,
Iwangoje Jehenamu, kiyama kikiingia,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!


Viongozi waadhimu, mnabadili tabia,
Sasa tunawatuhumu, mmekwishanunuliwa,
Na wengine wahujumu, dini yetu mwaiua,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!

Njaa imetakadamu, waoga wanunuliwa,
Bei rahisi adhimu, thamani wasiokuwa,
Hawajui umuhimu, Mola aliowajalia,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!

Utajiri kuukimu, macho hawajafungua,
Wakimbilia vidumu, hadi mapipa yajaa,
Hawa si waislamu, na kazi yao twaijua,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!

Wanasiasa haramu, bei wanajip0angia,
Ni wakubwa madhalimu, waiabudu dunia,
Na kinachowagharimu, ni viongozi kununua,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!

Amri hawasalimu, kwa Mungu tunayemjua,
Ila sasa madhalimu, Mola wao ndiye hua,
Tumwangukie rahimu, apate kuwaondoa,
Dini ikinunuliwa, wafuasi huburuzwa!

No comments: