Wednesday, December 28, 2011

Mwafrika anaweza

Kila ukimchunguza, Mwafrika anaweza,
Kuna kinachomlemaza, maisha yakamkwaza,
Hakuna anayewaza, jambo hilo kutengeza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Ukoloni wa kuzoza, watu walishamaliza,
Na tunachokibakiza, wakoloni waongoza,
Si watu wa kutengeza, bali juu kujikweza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Kuzalisha si waweza, ila kula na kusaza,
Ni watu wa kumaliza, wala sio wa kuanza,
Kazi ni kubangaiza, wala si nchi kugeuza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Sio watu wa kujaza, ila daima kupunguza,
Ni watu wa kupuuza, fanyeni mnayoweza,
Mzawa kimbia giza, mwenyewe kujiendeleza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Miaka mtamaliza, mbele hamtajisogeza,
Viongozi wana funza, hawawezi kuongoza,
Ukubwa kwao ni chaza, kuvuna wasichotunza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Someni mnaoangaza, na wengine kuwafunza,
Labda ije miujiza, Mzungbu keshawalemaza,
Neema itawaiza, kwa rushwa kuwapumbaza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Sifa wanaojijaza, kusonga hawataweza,
Watu wa kufululiza, wenyewe wakajikuza,
Hutuacha tulipoanza,kama si kutudumaza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Cha mzawa wanabeza, na Mzungu kumkuza,
Uchina inawabeza, na wengine kuwaiza,
Majuha wa kupumbaza, wengine wanawajuza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

Azizi unayeweza, tupe wasiolemazwa,
Nchi kuiendeleza, ugumu ukakatiza,
Ya heri kufululiza, hadi juu kutukweza,
Mwafrika anaweza, Mzungu kamlemaza!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: