Friday, December 23, 2011

Maradhi haya hatari

WALE wanaougua, vipimo visivyojua,
Kila wakijiangalia, wagonjwa wanadhania,
Maruerue yakawa, kazi nao kutembea,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Tabibu akichungua, hana anachogundua,
Na mgonjwa huzidiwa, machozi akayatoa,
Akalaani kwa ukiwa, shere akiihofia,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Mara utamsikia, kifua chaugulia,
Kisha kinamtambaa, na tumboni kuingia,
Mara kikaja kupaa, shingoni kikaingia,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Hapo hakitaishia, miguuni kitatua,
Na kisha kuendelea, mgongoni kikakaa,
Na dhiki kitamtia, na hofu ikamjaa,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Hili niliulizia, wazungu wakanambia,
Saikomatiki huwa, wao wanavyotambua,
Mtu anachougua, ni wasiwasi kumjaa,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Hofu ikamtambaa, na fikra kumvaa,
Kwa analolitarajia, huenda likatokea,
Hawezi chini kukaa,muda hautasogea,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Dawa yake sijajua, maana sikuambiwa,
Ila wenzetu najua, ushauri huutoa,
Waemao wa nasaha, 'mgonjwa' kumpatia,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

Ninawaombea dua, ahali pia jamaa,
Gonjwa wanaougua, Mungu kuwasaidia,
Nafuu kuwapatia, kawaida kurejea,
Maradhi hatari haya, kichwani yanayokaa.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: