Friday, December 23, 2011

Nesi na kabebwa twende

Nesi na twende sukuma, alipwe zaidi nani,
Shairi ninalituma, majibu myasaini,
Nchi naona nakama, sijui alipwa nani?
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Makilla sina kalima, naona uhayawani,
Mla sio mkulima, ila aliye mezani,
Naamini Yakarima, hili si yake imani,
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Hawa wanayoyasema, wanakosea anwani,
Barua yao kutuma, imekwenda ugenini,
Nchi iliyo ujima, unyonyaji mumiani,
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Na kama ni wanachama, chama chao si makini,
Kimekufuru nasema, na wezi waweka ndani,
Mapinduzi ni lazima, au twenda kitanzini,
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Naichelea nakama, watu hawatuamini,
Watuona ni dhuluma, tena ndugu na shetani,
Wao wazidi kuzama, sisi twajipa uzani?
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Ninakiomba chama, kiifanye tathmini,
Nesi na tunayemtuma, mwenye thamani ni nani,
Alipwe kubwa kasma, uhai anayeghani,
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Kubebwa wasiolima, nchi yashuka thamani,
Zimeshatota hekima, na busara mashakani,
Kama twataka uzima, haki budi kubaini,
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

Maisha sasa gharama, waumiao wa chini,
Enyi wetu waadhama, mkosacho kitu gani,
Mwala msichokichuma, hamwoni mwenda motoni?
Nesi na kabebwa twende, nani alipwe zaidi ?

No comments: