Sunday, December 25, 2011

Wananchi wape nyumba

Serikali Tanzania, kodi yenu inakuwa,
Kukusanya mwatakiwa, hazina ije kujaa,
Na kisha kuangalia, bora kwa Watanzania,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Ushauri mngejia, uzito ningewaambia,
Watu wanayongojea, unafuu wakajua,
Moja la kuanzia, wenyewe mwajifanyia,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Moja la kuanzia, wenyewe mwajifanyia,
Nyumba mwajijgengea, hata mwaka hamjakaa,
Sasa nawashangaa, wananchi kuwahadaa,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Ni hitaji kuanzia, la msingi lililokua,
Nyumba ukijipatia, mengine utajijua,
Afuteni hujijia, kwazo nyingi sana njia,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Kama kweli twanuuia, umaskini kuutoa,
Nyumba yapaswa ikawa, ndiyo iliyo bora njia,
Muda hautapotea, itakua Tanzania,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Usanii na sanaa, na watu kuwaimbia,
Hakutowassaidia, na janga kuwaokoa,
Lile linalotakiwa, watu nyumba nazo kua,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Akili mkitumia, deni kudundulizia,
Benki mkiziambia, hili hazitokataa,
Zitadai kuahidiwa, fedha hatiopotea,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Afya ya Watanzania kokote walikokua,
Mjini mtanyanyua, nako vijijini pia,
Ikawa shida kuugua, kwenye yetu Tanzania,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Elimu itasambaa, watu kupigania,
Nyumba itawafungua, mengi wakatarajia,
Na maisha bora kua, kitu cha kukimbilia,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Mipango itatufaa, nyumba zikipangiliwa,
Rahisi kuzifikia, kwa heri nayo mabaa,
Wengi tutawaokoa, hili tukidhamiria,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Maji vyanzo tukilea, nyumbani yataingia,
Na umeme nao pia, kuja hautochelewa,
Mashirika yatakua, kuzalisha na kutoa,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Barabara na mitaa, hali bora itakua,
Usafi utaenea, na uchafu kupungua,
Miji tutajivunia, na wageni kusimulia,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Watalii kutembea, kawaida itakuwa,
Waisifu Tanzania, utalii ukakua,
Mapato kuongezea, hazina kushehenea,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

Rabana twategemea, macho utawafungua,
Viongozi walokua, hili wakalitambua,
Kisha kulikubalia, na nyumba zikatimia,
Wananchi uwape nini, ukishindwa wapa nyumba.

No comments: