Wednesday, December 28, 2011

Wasema wanisaidia

Uongo unauzua, eti unanigaia,
Hicho unachochukua, na mimi najipatia,
Unaidanganya haya, mwananme usiokua,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Mola ninamuachia, dhahiri kukusikia,
Kisha akajipimia, ukweli uliokua,
Kitu sijashuhudia, ila maneno naambiwa,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Waema wanisaidia, maana nishalemaa,
Tumboni umevimbiwa, vyote umeshavitia,
Aibu ungelijaliwa, haya usingetwambia,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Haywani weza kuwa, ni bora waheshimiwa,
Kuliko uliyekua, uongoa uliyejaa,
Na mimi nakuumbua, chako sijakipokea,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Moto wajipalilia, hujui lakuongea,
Mdomo ukifungua, uongo unaachia,
Mkweli hukuzaliwa, siwezi kutazamia,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Ukubwa twakuombea, na nafsi ije jaa,
Imani hukujaliwa, chukua yako dunia,
Tutakuja kuamua, ukija tuamkia,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

Unaipenda dunia, haikupendi dunia,
Wewe waing'ang'ania, yenyewe itakuzoa,
Umejenga mazoea, mengine hutoelewa,
Wasema wanisaidia, kama wongo ulaniwe!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: