Wednesday, December 28, 2011

Titi la mzazi tamu

Asili kitu adhimu, kuilea ni muhimu,
Taifa kutakadamu, kiini kutohasimu,
Kamwe kisijidhulumu, kikose ubinadamu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Kiswahili lugha tamu, yatia wengi wazimu,
Ila walio dhalimu, lugha wanaihasimu,
Mengine watakadamu, ya kwao wanahujumu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Wasahau ukarimu, kwenu kwanza ni muhimu,
Amri wanasalimu, kwa yasiyo ya adhimu,
Wageuzwa maimamu, dini wasioifahamu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Ni chemchemi adhamu, kubeba yetu muhimu,
Mizizi kutakadamu, maarifa utakimu,
Vizazi vije kwa zamu, kujifunza yao amu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Uchina wanafahamu, lugha sio marehemu,
Hakika wameazimu, masomo kuikirimu,
Maarifa yametimu, ndani yake yatadumu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Ya kwetu kama wazimu, hapana wataalamu,
Haya hayagharimu, ila kwao si muhimu,
Wenyewe wajidhulumu, kizazi kitawahukumu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Mipango hawaikimu, na mikakati adimu,
Watu hawajirehemu, waendako hawafahamu,
Utumwa waukirimu, udumu daima dawamu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Laiti wangefahamu, titi la mzazi litamu,
Lingine halishi hamu, hatga unyonye kwa zamu,
Makusudio adhimu, yangelikuwa azimu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Nauliza wahujumu, Kichina sio muhimu ?
Na Kiarabu adhimu, au huu Uislamu?
Kiingereza adimu, kitazidi kutukimu?
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Haijawadia zamu, Kichina kusoma humu,
Na shahada adhimu, waende kutukarimu?
Magharibi yake zamu, haijesha umuhimu?
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

Ninakuomba Rahimu, nchi hii kurehemu,
Yaliyo kwetu adhimu, yawe mambo maalumu,
Yapatiwe umuhimu, hadimu usigharimu,
Titi la mzazi tamu, lingine laisha hamu!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: