Friday, December 16, 2011

Mtihani wa barua

Nashindwa andika barua, kisa teknolojia,
Vidole nishalemaa, kuandika nahofia,
Kompyuta yaua, uandishi kama sanaa!

Zamani nilitumia, kuandika kwa masaa,
Lugha kuidadavua, na nahau kutumia,
Na nyoyo nikazivaa, kwa murua ulokua.

Mashairi nilitia, katika zangu barua,
Mapenzi kuyalilia, na huruma kungojea,
Na vijisenti kutia, huba kuipalilia.

Majibu nilingojea, mapigo yakazidia,
Chini kushindwa kukaa, sijui pa kutembea,
KUisubiri barua, kama ilipokelewa.

Na nilipokataliwa, machozi niliangua,
Homa ikaniingia, kitandani nikatua,
Nje tena sikupajua, nikazidi kuugua.

Hawa aliposikia, mwenzie ninaugua,
Kisa yeye kuambiwa, huruma ilimwingia,
Majibu kunitumia, haraka kushadidia.

Nilitetema sikia, barua kuifungua,
Hilo sikutazamia, majibu kuja letewa,
Si kwa homa kuugua, ila kwa kufurahia.

Kisha nilipoyatia, machoni ya kuambiwa,
Machozi hujimwaia, aghalabu nikalewa,
Bahati kuingojea, ana kwa ana ikawa.

Barua hakika dawa, ambayo inapotea,
Mtu ukija ugua, tena hautojipatia,
KIsa teknolojia, sote tumeiridhia!

Tungo mpya 2011
Aina: Mitatu
© 2011 Sammy Makilla

No comments: