Monday, December 26, 2011

Kila giza likizidi

Hii ni yake tabia, tuijuayo dunia,
Uovu unapochanua, nuru inakaribia,
Wanapojaa wabaya, wema ndio wazaliwa,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Giza likipalilia, kila kona kuenea,
Mwanga nyuma hufatia, giza ukaliondoa,
Shari inapozagaa, heri njiani kuingia,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Ni ajabu ya dunia, ndivyo hivyo milenia,
Na wasiojielewa, njiani hukata tamaa,
Kumbe nusura hatua, wala haijafikia,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Ukweli ukiujua, subira utailea,
Na hatima kukimbia, mbaya iliyolaniwa,
Mustakabali ukawa, pepo kujipalilia,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Nchi inapojaa, machungu pia ukiwa,
Uongozi kutanua, na watu kuwasiginia,
Hufika wakati kuwa, afueni wakapewa,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Siri anayoijua, Muumba tu nakwambia,
Wengine watabiria, kile kisichotokea,
Na ya kwao kupangia, bahari kutarajia,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

Nilipo sijapajua, niendapo sijajua,
Ila ninachokijua, wajibu nimenuia,
Macho wote kufungua, dunia mkaijua,
Kila giza likizidi, nuru itachungulia.

No comments: