Friday, December 30, 2011

Hivi kazi nitapata?

Hivi kazi nitapata, mamangu hajulikani,
Barua nikizileta, kitu zitaaidia ?
Kitu gani nitaleta, hakika nayo nikawa,
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Ubavuni nikijata, kwa mama wa kufikia,
Hawawezi kunisuta, sio walionizaa,
Jina langu wakafuta, mitaani kutupiwa?
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Ubunge hakuupata, mama alipogombea,
Ufakiri kapakata, siwezi mtegemea,
Budi kazi kutafuta, pengine nitamsaidia,
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Hakujipaka mafuta, au mkorogo kutia,
Kwa watu hakunatanata, wakaweza mtambua,
Weusi ulimteta, mwangani hawakumjua,
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Uwaziri kaudata, kabaki kuusikia,
Na wakubwa hakuitwa, sio wa kuchagulia,
Umaskini anata, nani kumuangalia,
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Utajiri hakupata, ndugu kawasaidia,
Nyumbani tunachachata, mengi twabangaizia,
Walopata watusuta, nini tutawaambia?
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?

Najuta shemu Mjata, hali niliyofikia,
Nasaha naitafuta, waniachie na saa,
Twala wali wa mafuta, na nazi nilizoea?
Mamangu hajulikani, kazi naweza kupata?


© 2011 Sammy Makilla

No comments: