Wednesday, December 14, 2011

Bubu anapozomea

Yatakuja yakusibu, udhanie uraibu,
Wazungumze mabubu, tena wawe mahatibu,
KIsa chake ni dhahabu, alowalani Mujibu,
Usistaajabu bubu, kuizomea dhahabu!

Watayashika kwa ghibu, alama nazo hesabu,
Watafute majawabu, kuzipunguza ghadhabu,
Hapatakuwa muhibu, nchi hawataghilibu,
Usistaajabu bubu, kuizomea dhahabu!

Na hawa wastaarabu, wasio nayo aibu,
Wataja kuwaadhibu, waitambue adabu,
Kisa ni yetu dhahabu, kuipeleka janibu,
Usistaajabu bubu, kuizomea dhahabu!

Wataona wa ajabu, bibi na zao mababu,
Kila wakistaajabu, watashindwa uratibu,
Kwani hakuna majibu, ila ni tupu aibu,
Usistaajabu bubu, kuizomea dhahabu!

No comments: