Friday, December 30, 2011

Ujanja wenye hasara

Ajuaye kila kitu, ujanja wenye hasara,
Hujifukuzisha watu, mtu kujiona bora,
Na wengine ni kiatu, au bovu matambara,
Ujanja wenye hasara, ajuaye kila kitu!

Beleshi ndilo sepetu, gharama mwana hasara,
Hayendi maisha yetu, wengine wakisowera,
Hakuna kibaya kitu, kama bure masihara,
Ujanja wenye hasara, ajuaye kila kitu!

Usiache vifutu, kukufanyia duara,
Heri akumeze chatu, wasikunyanyase sira,
Maana kisu cha butu, hukuokoa kafara,
Ujanja wenye hasara, ajuaye kila kitu!

Ushauri jadi yetu, udikteta hasara,
Tusikilize wenzetu, haki bila kuwapora,
Tuijenge nchi yetu, kwa heri na takibira,
Ujanja wenye hasara, ajuaye kila kitu!

Swali jibu likifutu, hujitambua majura,
Wakarejea kwa utu, wajijengee mnara,
Usipotumia watu, itakudhuru hadhira,
Ujanja wenye hasara, ajuaye kila kitu!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: