Monday, December 26, 2011

Huwa ni nchi ya watumwa

Huwa ni nchi ya hadimu, lugha wasiotumia,
Amri wakasalimu, za wengine kutumia,
Huwa wajinywesha sumu, hali hawajatambua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Amri wanaosalimu, wakafata wajuao,
Huwa si wa kukimu, na sala si kazi yao,
Ni watu wa jehanamu, haya ni makazi yao,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Quran tukufu jua, hili inatuambia,
Mola alivyoamua, tofauti sisi kua,
Anataka hudumiwa, lugha tofauti kua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Vyuo vikuu mwajua, lugha inayotakiwa,
Kiswahili kukilea, anzeni kufundishia,
Mola atawasikia, na juu kuwanyanyua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Kiingereza chajikwaa, uzito unapungua,
Kichina kimeingia, Kijapani na kikorea,
Hili tusipoangalia, tutabaki kusinzia,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Watoto washindiliwa, wasopaswa kujua,
Miti ukiulizia, hakuna anayejua,
Samaki tunaovua, hakuna anayejua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Hata ndege nao pia, mitini wanaotua,
Hakuna anayewajua, ila ni kwa kudhania,
Wadudu utashangaa, wengi wasiowajua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Elimu si kupakia, ila yenye manufaa,
Elimu isiyokua, kwa lugha mama tambua,
Haiwezi saidia, matatizo kuondoa,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Utafiti huibiwa, wengine wakatumia,
Kwa lugha ngeni ukiwa, kila kitu chapotea,
Masikini twabakia, hata akili zaibwa,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Zinapotea dhahnia, dhana na keteze pia,
Nini tutakachogundua, wengine kuwauzia,
Au jalala tunakua, vya watu kuja mwagiwa?
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Watu wasiojitambua, mamlaka kuchukua,
Ni mzigo umekua, uoza tunaulea,
Nchi inahujumiwa, koloji jipya kua,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Wanaharakati radhia, kazi inawangojea,
Uongozi si kukaa, juu na ukubwa kuwa,
Ila watu kufanyia, wanayoyategenea,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Nchi mmekwishaachiwa, siasa zimefubaa,
Dini zachanganyikiwa, hazijui la kufaa,
Ubepari, ujamaa, hakuna kilicho dawa,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Wa kati mmebakia, gozi kutukokotea,
Mchazo safi ukawa, na magoli kupatia,
Ikang'aa Tanzania, iache kufubaa,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

Utumwa huu mbaya, lazima kujiokoa,
Ya Mola kuyatambua, tofauti kuzijua,
Heri kuisimamia, lugha budi kutumia,
Huwa ni nchi ya watumwa, lugha yao waachao!

No comments: