Monday, December 26, 2011

Hii ni tamu ya ndoa

Mwenzio hutamjua, kila anachofikiria,
Hilo ukilitambua, mengine unaachia,
Hukubali majaliwa, na kile kitakachokua,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Haiwi mkawa kimoya, ni viwili vinakua,
Mwenzio anachojua, sicho unachokijua,
Na akli sio sawa, wengine wanazidiwa,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Imani waliojaa, Mola kuwatangulia,
Sala wanaozijua, kwa wakati kutimia,
Na dua wanaotoa, muafaka na sawia,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Ibada waliojaa, na Mola kumwangukia,
Vitabu kujisomea, vitukufu vilokua,
Nuru huwatangulia, yalo bora kuamua,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Wajibu huutambua, na haki hatochagua,
Na mema hukazania, baraka zikaingia,
Huruma huwa wajaa, wengine kusaidia,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Na mengi huyagundua, ndoani yasiyofaa,
Wakajifunza radhia, kutenda na kuamua,
Na siku zote mashallah, kweli hawatachelea,
Hii ni tamu ya ndoa, vinginevyo haikai.

Ndipo nikawafunulia:
Akipanda wewe shuka
Akifukua wewe zika
Akifoka wewe toka
Akibweka wewe wika,
Akijifanya mzuka
Wewe kitanda tandika
Na kisha lala na kuamka
Salama utasalimika!

Na tena:
Ulimi silaha mbaya,
Mwenye nayo humuua,
Adawa akabakia,
Ulimi unabomoa,
Juu hautakunyanyua
Ila ukishaamua
Kwa heri kuutumia
Hata nyoka humtoa
Pangoni alimokaa
Na mwenye nia mbaya
Wa kheri mtu kuja kuwa!

1 comment: