Friday, December 16, 2011

Utu unapopungua

Utu unapopungua, hayawani watu kua,
Huruma huchechemea, na imani kulemaa,
Ubinadamu huvia, na uungwana kupwaya,
Katika yao dunia, watu hofu huwajaa,
Utu unapopungua, hofu watu huwajaa!

Utu unapoenea, kuaminiana dawa,
Pahala usipokua, huwa kwetu mbaya dua,
Tuhumu huzizindua, wahaka pia nazaa,
Na kuchagiza balaa, nuksi na mikosi pia,
Utu unapopungua, hofu watu huwajaa!

Utu kutojipendelea, nafsi kuabudia,
Wewe na wako jamaa, uungu mkajautwaa,
Hung'aaka Adilia, juu chini kuwang'oa,
Tazama kule Libya, yaliyokwishakutokea,
Utu unapopungua, hofu watu huwajaa!

Utu ni kufikiria, na sio kung'ang'ania,
Hekima ukaihadaa, na busara kuiumbua,
Hapendi aliyekuwa, Muumba wa hii dunia,
Na akikukasirikia, hakika umepotea,
Utu unapopungua, hofu watu huwajaa!

Nani kutuhurumia, Murtaali na Alaa,
Hazikutoshi kofia, za ulimwengu kuvaa,
Ni mengi unayoyajua, sisi tusiyoyajua,
Na hakika yetu njia, mwanzo na mwisho wajua,
Utu unapopungua, hofu watu huwajaa!

Tungo mpya 2011
Aina: Mitano
© 2011 Sammy Makilla

No comments: