Monday, December 26, 2011

Marafiki wa shetani

Marafiki wa shetani, hawakai penye jema,
Kazi yao uzaini, ukweli hawatasema,
Usiku ni mumiani, machana ni watu wema,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Ufasidi ni auni, huwasaidia njama,
Mikakati wakibuni, imefurika dhuluma,
Mipango yao uhuni, nchi na watu hukwama,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Tasnia wakibuni, himaya hujijengea,
Waishi wakiamini, hawatakutangulia,
Awasgabgaa Manani, ruia haziamini,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Nawe usiwaamini, au watakutumia,
Hiyo ndiyo yao dini, wataka kuabudiwa,
Ukimkana shetani, hatia watakutia,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Wapo tele waumini, na viongozi wajaa,
Anzia misikitini, hadi kanisani pia,
Wanafiki kwa yakini, Muumba keshawaumbua,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Hugeuza duniani, pepo yao ya kukaa,
Wakamdhihaki Bathini, kiyama kukitania,
Na wengi hujiamini, kumbe wameshapotea,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Wakiitwa mashakani, kama watoto hulia,
Daima hawaamini, dunia itawakataa,
Mateke wakibaini, mshtuko huwaua,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Siku hawaiamini, Ziraili akitua,
Kisha huganda moyoni, na mwilini nako pia,
Mate huisha kinywani, na kauli kupotea,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

Awe adui shetani, Mola ikubali dua,
Niepushe mitihani, salamani nikakaa,
Mwisho uwe ni auni, daraja linalofaa,
Marafiki wa shetani, huogopa malaika.

No comments: