Friday, December 30, 2011

Msomi hathaminiwi

Hana kabisa thamani, wengine waogopewa,
Nani anayemwamini, shauri akalipewa,
Wote kwao mashetani, wao malaika wawa,
Msomi hathaminiwi, ndio yetu Tanzania!

Maamuzi yote nchini, wabovu wanatumiwa,
Na kilichokuwa duni, ndicho kinaamuliwa,
Kuuaga umaskini, hii nasema ruia,
Msomi huogopewa, ndio yetu Tanzania!

Ugiriki tazameni, zamani ilivyokua,
Uchina nako Romani, maamuzi wakitoa,
Ya wasomi ni amini, hayaachi kutumiwa,
Msomi hathaminiwi, ndio yetu Tanzania!

Na unayemthamini, haachi bora kuwa,
Mataifa duniani, hili wanalitambua,
Ni matofali auni, nchi kujaijengea,
Msomi huogopewa, ndio yetu Tanzania!

Akili walio dunia, hili hawatalijua,
Vingine hujiamini, hadi wakatumbukia,
Kulikoni mashimoni, vigumu kuokolewa,
Msomi hathaminiwi, ndio yetu Tanzania!

Ila walio makini, hili wanalielewa,
Wasomi huwathamini, na yao wakasikia,
Na kisha hutathmini, yalo bora kuamua,
Msomi huogopewa, ndio yetu Tanzania!

Nchi huwa mashakani, kuwa na wanaojua,
Kila kilicho uzani, maamuzi kuchukua,
Nchi huja walaani, wasiwe wa kukumbukiwa,
Msomi hathaminiwi, ndio yetu Tanzania!

Wape wetu wahisani, akili ziiizokua,
Waweze kuwaamini, washauri wa kufaa,
Nchi ipate thamani,kwa kile inachotumia,
Msomi huogopewa, ndio yetu Tanzania!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: