Friday, December 30, 2011

Hutaniwa tasnia

Kazi nyingine yafaa, sio ya kusimulia,
Ukweli inatakiwa, sio uongo kuuzua,
Mambo kujipikia, yasiyokuwa yakawa,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Kafiri kutumikia, mwandishi anapotea,
Heshima hujivunjia, akakosa kuaminiwa,
Utu huja kupotea, ovyo kudharauliwa,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Uandishi kujijua, na wito kuupokea,
Wanyonge kusaidia, na sio kusaidiwa,
Hapo ukipafikia, mbele hautaendelea,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Kiatu lazima kuwa, kafiri wakakuvaa,
Mavi kuyakanyagia, wewe wakakuachia,
Na waliokutegemea, vingine kukuelewa,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Wito ungepigania, nyuma wangelibakia,
Kambi ukiikimbia, muasi watakujua,
Usemalo hupotea, masikio kuzibia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Dini budi kurudia, utuwe ukaujua,
Kwako kuyaazimia, watu yatayowafaa,
Hatua ukachukua, kufata adhimu njia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Njia usiyopotea, Muumba akaridhia,
Kwa yakini kukulea, kilicho bora ukawa,
Jina akakujengea, na kizazi kufatia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Mtumwa mwenye hadaa, kingine hawezi zaa,
Hata vipi akikilea, ovyo lazima kikawa,
Uhuru hatoujua, hadi mwisho wa dunia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Enyi mliopotea, ombeni kujitambua,
Pumzi kuhesabia, neema mliyojaliwa,
Si ovyo kuitumia, mkaja kuyajutia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!

Ibariki tasnia, wenye wito kuingia,
Wanyonge kupigania, haki wakajipatia,
Fukara kuwainua, na sisi kujipatia,
Hutaniwa tasnia, kafiri kutumikia!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: