Wednesday, December 28, 2011

Msingi umeshajengwa

Uchina na Malaysia, mamao wanamlea,
Tena wanajivunia, wazidi kuendelea,
Hatua waliyofikia, mama kawasaidia,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Majuha tuliokua, ung'eng;e twang'ang;ania,
Twadhania ni dunia, Kiingereza kujua,
Nchi zinadidimia, tutakujajionea,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Jioni imeshakua, magharibi yaingia,
Mashariki laanza jua, ndio kwanza latokea,
Na kwa wanalojijua, hili wataling'amua,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Mashariki kunafaa, kwenda kujinyanyua,
Magharibi kutembea, wataali kuja kuwa,
Vichache kuokotea, vya kuja kujazilia,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Hivyo tungelianzia, nyumbani kutia paa,
Kiswahili jua kua, havi vyuo kutumia,
Na kisha kufyonzea, maarifa yakakua,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Uchina ninawaambia, elimu zote watia,
Kwenye lugha watumia, kwa kazi na kufundishia,
Hakuna wasilojua, na wengi hawajawajua,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Malaysia nao pia, lugha wameipania,
Kote wanaitumia, toka huko chekechea,
Nini utachowambia, ksiwe kimalaysia?
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Sisi mama twamchezea, kwa rushwa kuzipokea,
Lugha kutoitumia, Kiingereza kubakia,
Hali wote tunajua, wazito kushikilia,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Ilivyo sasa dunia, lugha zao watumia,
Kisha wanazifungua, maabda zikajaa,
Lugha kufundishia, mbalimbali zilokua,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Lugha wana huchagua, ipi ya kuichukua,
Mbili tatu zinakua, zote vyema akajua,
Maabara hutumia, miezi michache waa,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Kizamani twabakia, miaka kuitumia,
Wenzetu fumba fumbua, lugha mpya hujua,
Maabara kutumia, shuleni zinazokaa,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Mkakati hutumia, dunia kuangazia,
Wapi kunakofaa, bidhaa kuzichukua,
Na elimu kuitwaa, enzi inazozifaa,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Ila budi kujaliwa, viongozi wakufaa,
Baraka wanaochukua, na uchaMungu kupewa,
Majina watakapewa, nyuma yawezayo bakia,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Na sio wapita njia, waigizao sanaa,
Wamekuja kutumia, na matumbo kuchumia,
Na sio kutumikia, watu wakawanyanyua,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Bishara ukizijua, Mola hukufunulia,
Za kuzipitia njia, watu uje kuwafaa,
Na lugha yao kukua, ikaikubali dunia,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

Aidhawanaotubia, naye kumgeukia,
Rehema zimemjaa, na huruma kajaliwa,
Wadogo huwasikia, kama wakubwa wakiwa,
Msingi umeshajengwa, nani kuendelea?

© 2011 Sammy Makilla

No comments: