Friday, December 23, 2011

Wanaolisha uoza

Waishio kwa tamaa, haramu wakavamia,
Uoza huupakua, wakawalisha jamaa,
Chumo wakajichumia, moto linalouvaa,
Wanaolisha uoza, huwa karamu ya funza!

Laiti wangelijua, u0za wangekimbia,
Mafunza huwapokea, na wakasherehekea,
Karamu kujifanyia, mzoga wanapokua,
Wanaolisha uoza, huwa karamu ya funza!

Na wadudu kila baa, maiti hushambulia,
Baadhi huwa wakataa, ulivyokua kinyaa,
Watu bora kungojea, miski wakawatia,
Wanaolisha uoza, huwa karamu ya funza!

Nyama unajichomea, huku fika unajua,
Kuoza imeshakua, biashara wajitia,
Na kisha kusingizia, hasara waikimbia,
Wanaolisha uoza, huwa karamu ya funza!

Manani keshatuambia, kilicho bora kutoa,
Hata watu wakijua, aliamini ukawa,
Heshima kukutangulia, hata siku wajifia,
Wanaolisha uoza, huwa karamu ya funza!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: