Wednesday, December 14, 2011

Kupenda chako kwa dhati

Pasiwe vigezo pacha, kwa wako na muminati,
Ujue hapatakucha, akiwemo afriti,
Hufanza mengi kuficha, ukawa uso bahati,
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!

Iwe kwa meno na kucha, malezi yawe ya dhati,
Si kwa baki kuwaacha, wako ukawaneemati,
Manani hutamficha, mtihani wasaliti,
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!

Iwe ni ya kweli picha, si igizo mahluti,
Pasiwe unalokacha, ya heri ukatafiti,
Wote kutokuwaficha, ya kuwajenga kwa dhati,
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!

Maisha sio mchicha, yana kazi na bahati,
Yenyewe ukiyaacha, yatamhini Muhiti,
Yarabi wanaomcha, kwa hili hawatakati,
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!

Lukman sitamwacha, mafunzo yake mukliti,
Alifikiri kwa kichwa, si kwa moyo na manoti,
Kwa wanawe kawa Kocha,kuwafunza ya Muksiti,
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!
Kupenda chako kwa dhati, kiwajibishe zaidi!

No comments: