Monday, December 26, 2011

Ubaguzi sio rangi

Twenda tajirika kwao, lazima kutubagua,
Ni wao walimao, kuvuna twawaingilia,
Pamoja na waibao, kama Australia,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Tunangoja kwenda kwao, ndio tupate kung'aa?
Sisi sio wapandao, kwetu vitu vikakua,
Twawategemea wao, ili tupate kujaa,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Hatutunzi wachezao, Afrika yenye njaa,
Hadi waende makwao, ndipo wanapo wanyanyua,
Si watu watetao, hadi kwao kuingia,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Magazeti na redio, huwapamba wakang'aa,
Bila kula walavyo wao, ingesinyaa afya,
Kwetu wote waombao, hakuna kujitegemea,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Kwetu kote ni wafao, kwa kiu nayo njaa,
Ni tuwategemeao, ili letu likakua,
Na wao ni wajuao, ukweli wanatuambia,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Na nje ni wajuao, viongozi walokua,
Hapa kwetu waibao, na kwao wakafichia,
Ndio wawashangaao, ujinga tunaolea,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Laiti ingelikuwa, masikini hatukuwa,
Mali asili jaliwa, wote sisi yatufaa,
Kila mtu anajaa, sio majuu kujaa,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Kila mtu anajaa, sio majuu kujaa,
Wenyewe tunatumia, sio tunawachumia,
Na wala sio wenye njaa, makombo kuombewa,
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

Wazungu wangeingia, maboi kwetu wakawa,
Nyumbani kuwatumia na barabara kufagia,
Ubaguzi ungekua, wa mzungu au mzawa?
Ubaguzi sio rangi, ubaguzi ufukara!

No comments: