Wednesday, December 28, 2011

Uchina na Malaysia

Ukienda kwao jua, hili utafurahia,
Lugha wanajivunia, shuleni kuitumia,
Na vyuo vinachanua, lugha wanairingia,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Sitini tulianzia, masikini tulikuwa,
Wao walishang'amua, tatizo lililokua,
Wakalishughulikiwa, sawaswa kuliua,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Lugha walishatambua, si yao kuitumia,
Hivyo wakajaamua, makosa kuyaondoa,
Wakajipanga shujaa, elimu iwe kizawa,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Wachina wakachanua, vitabu kujitungia,
Kichina vikitumia, ili kuja fundishia,
Miaka hawakuchukua, kila kitu wakajua,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Wenzetu Malaysia, hayo waliyaamua,
Wakajitafsiria, kila wasichokijua
Kimalysia kuchukua, maarifa ya dunia,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Sasa lugha watumia, yao wenyewe wazawa,
Kila somo wanajua, kwa kazi na kufunzia,
Nchi yao inakua, dunia ya pili yawa,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Twadanganywa Tanzania, lugha ngeni kutumia,
Muda wazidi potea, nchi inachechemea,
Laiti tungelitumia, mbali tungelishakua,
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!

Kujiuliza yafaa, elimu kwani ikawa?
Kama sio kutatua, matatizo yalokua,
Na fursa kutumia, ili watu kwendelea?
Uchina na Malaysia, lugha wanajivunia!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: