Friday, December 30, 2011

Umeme twausikia

Uhuru tunaujua, tena tumeshaugua,
Vinazidi vitambaa, njiani kuupepea,
Twahofia kupotea, umeme msipotuwashia,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Uhuru twautambua, ila giza laingia,
Umeme mngetuwashia, mengi tungejionea,
Kama hivyo haikuwa, tunaenda kuvumbua,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Ahadi mmezitoa, au pipi mmezigawa,
Akili mwatuchezea, au shere imekua,
Vipi mwajisikia, mabomba mkimwaia?
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Mchuchuma naelekea, mkaa kujiokotea,
Nyumbani nitatumia, umeme sawa ikawa,
Nachoka vumilia, miaka yatangulia,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Dini mnaoijua, ibada mngefanyia,
Moto kuugharamia, waumini kutumia,
Sio sadaka kutwaa, wenyewe mkajilia,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Mwafanya yasiyofaa, uchaMungu mwajitia,
Laiti mngetambua, kile kinachowangojea,
Mbali mngesogea, na wanaowahadaa,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Watu mnawakimbia, wakubwa mwawafanyia?
Hivi Mola mtamjua, kwa watumwa nyie kuwa,
Au viongozi kuwa, ukweli mkatetea?
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Uhuru babu mwajua, wao waliulilia,
Nyie sasa mwaua, hata walichoanzia,
Aibu ingewajaa, ghafla wangetokea,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!

Masikini walokua, chini yenu watembea,
Hivi mwawaangalia au mnawasiginia?
Mola ninamlilia, ya kwenu kuwagaia,
Uhuru tunaujua, umeme twausikia!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: