Chumba cha masononeko, furaha ndani haiko,
Heri humo huwa mwiko, kila siku sikitiko,
Hakuna mwenye ujiko, wachache hukaa huko,
Chumba cha masononeko, ni chumba katika giza!
Huvuka vingi vivuko, ukija hapo vituko,
Ukiupata mwaliko, kaugange moyo wako,
Kunao mfadhaiko, usipate mshtuko,
Chumba cha masononeko, ni chumba katika giza!
Mama kafunge mbeleko, uzazi una mauko,
Hutesa manung'uniko, kwa mengi mahangaiko,
Hugura zote chereko, uwe kama mbwa koko,
Chumba cha masononeko, ni chumba katika giza!
Usininyime kicheko, muumbaji wa vituko,
Nipe lako farajiko, hata panako maziko,
Kilio kisiwe shtuko, ila shukrani kwako,
Chumba cha masononeko, ni chumba katika giza!
© 2011 Sammy Makilla
Friday, December 16, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment