Monday, December 26, 2011

Uongozi ni wa nini?

Uongozi nahofia, wivi waweza ukawa,
Kama wanaojipatia, wakubwa waliokuwa,
Wanyonge kudhulumiwa, na kidogo kuchukuliwa,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Kiongozi akipewa, milioni kwa mamia,
Na hawa nao raia, kumi hawajaijua,
Huu sio wizi hua, mchna waendelea?
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Kumi na nane saa, daktari atumia,
Wagonjwa kuhudumia, bila hata kupumua,
Twashindwa kuwaangalia, wenyewe twajiangalia?
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Nesi kote huingia, haishi kujichafua,
Matapishi hufadia, na vinyesi kuchukua,
Bungeni unayekaa, chote hicho wachukua?
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Mwalimu choki yaja, machoni na kwenye pua,
Elimu anaitoa, kesho watakaomnyonyoa,
Hili twaliangalia, tunashindwa kuamua,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Sahani mbili mwatwaa, tonge hatujalijua,
Na kisha mwagugumia, hakiwatoshi mwaonewa,
Ibilisi mmekua, binadamu twadhania?
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Kipimo mnachotumia, mimi bado kukijua,
Kiasi gani mwatwaa, na kiasi gani mwatoa?
Nini mnakichukua, na nini mwatupatia?
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Au mwavuna mamia, hata msikopandia,
Kwingine mwakupua, vya wengine vilokua,
Hakika nawashangaa, watu msiojijua,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Kwa haya mtachukia, ukweli nawaambia,
Mungu mkimtambua, mtageuka tabia,
Nafsi kuzizuia, wengine kuwatangulia,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Tazameni Malaysia, zamani walipoamua,
Viongozi kukataa, malipo yaliyozidia,
Wananchi kwanza kupewa, mtaji wakaendelea,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Kisha wao kufatia, nchi imeshanyanyuliwa,
Nyie mwanza kutwaa, nchi inadidimia,
Na Mola kawaumbua, mafuriko kutokea,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Sasa tunawashangaa, mwashindwa wajengea,
Hivi mnategemea, muujiza kutokea,
Fisadi walizochukua, kwanini kutotumiwa,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

Nyumba ninawaambia, kwa fakiri ndio dawa,
Hili ukishampatia, mengine atajijua,
Ila mkiliachia, dhulumati tatajua,
Uongozi ni wa nini, kama watu hawapati?

No comments: