Monday, December 26, 2011

Figo hazifanyi kazi

Figo hazinayo kazi, hustahili kuwa nazo,
Watakiwa uamuzi, kuuongoa mzozo,
Apatikane mchuuzi, akufanyie mauzo,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

Usiifanye ajizi, zitakwisha pumzizo,
Ubakie ni wajuzi, kwenye haya mazungumzo,
Hali ilikuwa wazi, siku ulikuwa nazo,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

Halihitaji ujuzi, liwazi tokea mwanzo,
Ukifanya ubazazi, hufanywa ya mawe nguzo,
Ukabaki simulizi, au pengine tangazo,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

Yatakiwa mageuzi, na sio mazungumzo,
Maneno ni upuuzi, zama hizi za chetezo,
Moshi haunao kazi, yatakiwa ya mkazo,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

Alama zashehenezi, au kwako maigizo,
Hii ngoma ya maswezi, eti kwako ni mchezo?
Isiwe hatuyawezi, pakatokea uozo,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

Mengi yataka kimbizo, mwenzetu wazidi pozi,
Hulijui shinikizo, halinalo kizuizi?
Usituseme kikwazo, kumbe wewe kizuizi,
Figo hazifanyi kazi, wang'ang'ana kuwa nazo?

No comments: