Monday, December 26, 2011

Wahariri wanaua

Wahariri Tanzania, mashairi wanaua,
Fani wanyanyapaa, imebakia ukiwa,
Washairi wanalia, wapi wende kuhamia?
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Rai na Mtanzania, kama hivi hamkua,
Uhuru mnazidiwa, hamu inatupungua,
Mwananchi mwasuasua, yakini hatujajua,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Tanzania daima pia, pembeni twapembuliwa,
Mzalendo lafifia, imebaki kusifia,
Nipashe si tena shua, vingine mnaamua,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Majira tuliyoijua, ni jina limebakia,
Sanaa ilikoanzia, ndiko sasa inafia,
Laiti wangetambua, yapasa kule kurejea,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Wadaku wanaodakia, kudokoa wazoea,
Utitiri umejaa, maudhi isofaa,
Nchi bado yawalea, kubaya twaelekea,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Redio zimesheenea, mashairi wazuia,
Sipati kuyasikia, wala kuzungumziwa,
Lugha wanaoiua, ushairi waanzia,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Televisheni zajaa, ushairi wafukiwa,
Hakuna historia, wala mfano wa sanaa,
Ya nje twayasikia, ndani yadharauliwa,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Tovuti naitumia, hifadhi bora ikawa,
Nyuma wakiifungua, sanaa watafukua,
Kimya hatukukaa, wengine tuliyatoa,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

Ushairi ukivia, lugha nayo hudumaa,
KIsha huweza lemaa, isije tena kukua,
Watu wabaki kulia, hakuna cha kuokoa,
Wahariri wanaua, sanaa hya mashairi!

No comments: