Thursday, December 22, 2011

Machozi ya kisiasa

Unafiki umejaa, siasa tunazolea,
Wajua lisilofaa, bado waliitikia,
Kisha na wewe walia, maafa yakitokea,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Mangapi tunayajua, ni hatari yalokua,
Bado twayaangalia, hakuna wa kukemea,
Kisha likizuka baa, ndio wa kwanza kulia,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Ni chafu hali ya hewa, badala ya jua mvua,
Tsunami twasikia, pengine yanyemelea,
Bado hatujaamua, mauti achekelea,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Uongozi wasinzia, jengoni na nje pia,
Nami sintoshangaa, kwa yatakayotokea,
Uongo sintolia, kimya nitanyamaa,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Uongozi ninajua, daima kutangulia,
Njia ukazitambua, kupita zinazofaa,
Na pabaya kupajua, kwenda ukawazuia,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Je, wanaowaachia, wananchi wakapotea,
Na kisha wakanyamaa, hadi izuke balaa,
Hawa kweli wanafaa, viongozi wetu kuwa?
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Twafanya tusiyojua, twaacha tunayojua,
Kichekesho kimekua, sinema yaendelea,
Mchunga ahadaiwa, kondoo wazidi kuliwa,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Rabana karibu kaa, uongozi kukwachia,
Viranja wanunuliwa, rushwa inaota mbawa,
Uongo sasa ni dawa, viongozi watumia,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

Tupe yanayotufaa, na shetani kumwondoa,
Nchi ije tengemaa, dua kuzikubalia,
Hatua tukasogea, akhera na kidunia,
Huwa machozi ya mamba, machozi ya kisiasa.

No comments: