Wednesday, December 28, 2011

Ninataka nikumbukwe

Nisikumbukwe vingine, katika hii dunia,
Zaidi watu wanene, ukweli niliulea,
Na kwa adha na mavune, daima sikuachia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Moja haikuwa nane, kwa nilivyoshuhudia,
Nane haikuwa nne, watu nilipowaambia,
Na mwembamba si mnene, katu sikumsifia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli!

Naomba nisiubane, upana uliokua,
Na ukweli niuone, hata gizani ukiwa,
Wazaini niachane, hata nisipoambua,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Nijaliwe tu kichane, mavuno ninayopewa,
La msanii nisisane, niwaachie vichaa,
Niukubali ujane, siku unaponijia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Nifanyanyo kifane, watu kikawasaidia,
Wanaokonda wanone, kwa siha pia afya,
Wasioona waone, na viziwi kusikia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Wanaoumwa na wapone, hata bila kutibiwa,
Uwalii nisigune, jina nikikabidhiwa,
Yafumukayo nishone, nisiachie kuachia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Kumbikumbi na senene, nyumbani kutumbukia,
Njia wenyewe waone, bila kuwafuatia,
Utukufu niuone, kwa kila ninachopewa,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Wakiwashwa niwakune, utulivu kuwajia,
Wenye vidonda nishone, kwa mate kuyatumia,
Na asali niirine, na watu kuwapatia,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

Nilichopanda nivune, zaidi kutochukua,
Kisicho changu nikane, wenyewe kuwaachia,
Nafsi yangu inene, kweli dahari ikawa,
Ninataka nikumbukwe, nilikuwa ni mkweli.

© 2011 Sammy Makilla

No comments: