Friday, December 30, 2011

Mgonjwa umembeba

Hofu inakutambaa, hadi machoni yang'aa.
Sababu sijaijua, au uliyemchukua,
Waogopa kukufia, njiani bado ukiwa?
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Dhamana umechukua, tena umezidishia,
Ni vigumu kutulia, acha mbali kupumua,
Mikono imekujaa, lipi kuachilia?
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Ukubwa mwaulilia, kiasi hamjajua,
Na yanapowaelemewa, sababu ovyo mwatoa,
Na majibu ya kinyaa, utu yasiyojaliwa,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Mgonjwa mwamchkua, kavukavu imekua,
Machela kugharamia, mmeona ni udhia,
Au mmepungukiwa, michango haikutimia?
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Ambulensi mwaachia, mjini kutembelea,
Kijijini kufikia, ni vigumu haijawa,
Mwasema mmeendelea, njia gani mwatumia?
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Haya mgonjwa alia, spitali kufikia,
Vipi mtakimbilia, yasishe yake masaa,
Au mtaadhiriwa, njiani aje wafia?
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Zaidi mlizubaa, mgonjwa kumchungua,
Saa hizi angekuwa, dokta keshamwangalia,
Ugonjwa umezidia, hatihati imekua,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Chakula hakupatia, atembea nayo njaa,
Maradhi yanaingia, hadi yasikotakiwa,
Kazi kubwa itakuwa, mgonjwa kumfufua,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Chakula ulijilia, chote alichopikiwa,
Uzito ulijitia, kujabeba hukujua,
Hakika nawashangaa, juu mlotangulia!
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Wenyewe mwajipalilia, wananchi wateketea,
Kinyume ngetarajia, watu kwanza kuwagea,
Kisha ndiyo ije kuwa, na nyie kujimegea,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Wa kwanza mmeshakua, kila kitu kupakua,
Unga ulipoishia, mchuzi mkaumwaa,
Hakuna kilichobakia, sufuria zinang'aa,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?

Iweje mnashangaa, mgonjwa keshazidiwa,
Haya mmemtakia, shari yenu ilokuwa,
Na njiani akiwafia, haki yenu itakua,
Mgonjwa umembeba, waogopa kukufia?


© 2011 Sammy Makilla

No comments: