Wednesday, December 28, 2011

Shaaban Robert

Laiti ungelizaliwa, nchi isiyolaaniwa,
Ubinafsi iliyojaa, wenyewe wanajifaa,
Wao wanapojifua, wengine wanafulia,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Hii leo ungekuwa, ni wetu Shakespeare,
Jina lingenyanyuliwa, kwenye minara likawa,
Kumbukumbu kujengewa, na vitabu vikajaa,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Kubwa lingelikuwa, Kiswahili kuenziwa,
Leo kingelitumiwa, vyuoni kufundishia,
Mbegu tukajipandia, asili zinazofaa,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Watumwa tusingekuwa, wengine tukawafaa,
Wavune wasichosia, na vyetu kuvichukua,
Vyote tungehifadhia, fasili ikavilea,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Nchi yazainiwa, ugeni kuutambia,
Rushwa inatumiwa, Kiingereza kukaa,
Na wajinga walokua, wadhania kitakua,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Giza laanza ingia, magharibi ilokua,
Hakuna anayejua, muda litakalokaa,
Ila kwa wanaojua, matlai wahamia,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Uchina ungefufuliwa, mwenyewe kujionea,
Lugha wanaitumia, na nchi yazidi kupaa,
Na huko Malaysia, nao wanaendelea,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Ni sisi tunakosea, njia tunayopitia,
Ujibari twajitia, taabu kukosolewa,
Ni ndoto ninahofia, umaskini kuondoa,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!

Usiache omba dua, wenyeji kuwazindua,
Wajifanya wanajua, kumbe wote ni majuha,
Bishara kutuombea, viranja wanaofaa,
Shaaban Robert, kwenu hauthaminiwi,
Mshairi na mtunzi, dunia itakuenzi!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: