Sunday, December 25, 2011

Shetani kakupa mwana

Hili nimefikiria, malenga nawaambia,
Sasa nawaelezea, mpate nifumbulia,
Nini kitakachokuwa, na ytakayonitokea,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Huruma katuonea, mwana kutokujaliwa,
Na katunong'onezea, dawa yeye anajua,
Bure atatupatia, tusiache kutumia,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Tamaa ikatuvaa, huku tukimwaminia,
Kwa kuwa atuhurumia, nia njema nayo kawa,
Pamoja kumwitikia, haraka katuletea,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Mwana tumeshajaliwa, ila bado twachungua,
Kiumbe aliyekua, kama mtu atakua,
Au shetani tumezaa, dunia kuitania,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Hakika ninahofia, wenzangu na wao pia,
Mazuri tulidhania, yatakuja kutokea,
Sasa kinachoendelea, majibu hatujajua,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Kwani tulifikiria, Mola katukubalia,
Na heri katuridhia, atatuonyesha njia,
Katikati kuingia, twakuta tumepotea,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Hatujui tumepewa, au tumechukuliwa,
Twaona kama twapaa, lakini tunatembea,
Hadithi zasimuliwa, hii ya shetani njia,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

Ofisi keshafungua, nyumbani keshahamia,
Na yote yanayotokea, ni yeye anayeamua,
Pembeni twasukumiwa, umeshaanza ukiwa,
Shetani katupa mwana, binadamu atakua?

No comments: