Friday, December 30, 2011

Uhuru tunaujua

Uhuru tunaujua, tena tumeshaugua,
Vinazidi vitambaa, njiani kuupepea,
Twahofia kuungua, maji yasipotolewa,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Uhuru twautambua, ila kiu twasikia,
Maji mngetupatia, zaidi tungesikia,
Kama hivyo haikuwa, tunaenda kuchimbua,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Ahadi mmezitoa, au pipi mmezigawa,
Akili mwatuchezea, au shere imekua,
Vipi mwajisikia, mabomba mkimwaia?
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Kisimani naelekea, maji kwenda jichotea,
Hii leo Ijumaa, suna inashauriwa,
Maji kuyatumia, hadi ya kuyaogea,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Dini mnaoijua, ibada mngefanyia,
Maji kuyagharamia, waumini kutumia,
Sio sadaka kutwaa, wenyewe mkajilia,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Mwafanya yasiyofaa, uchaMungu mwajitia,
Laiti mngetambua, kile kinachowangojea,
Mbali mngesogea, na wanaowahadaa,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Watu mnawakimbia, wakubwa mwawafanyia?
Hivi Mola mtamjua, kwa watumwa nyie kuwa,
Au viongozi kuwa, ukweli mkatetea?
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Uhuru babu mwajua, wao waliulilia,
Nyie sasa mwaua, hata walichoanzia,
Aibu ingewajaa, ghafla wangetokea,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!

Masikini walokua, chini yenu watembea,
Hivi mwawaangalia au mnawasiginia?
Mola ninamlilia, ya kwenu kuwagaia,
Uhuru tunaujua, maji hatujayajua!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: