Wednesday, December 28, 2011

Siri ya maendeleo

Lugha isipotumiwa, yakini kufundishia,
Nchi haitaendelea, wala kuja fanikiwa,
Matatizo yatakua, mikosi pia balaa,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Watawala walokuwa, wanadhania wanajua,
Kumbe mbali wapotea, na kuisahau njia,
Katu hawatatusaidia, ila watajisaidia,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

WATU waliojaliwa, lugha yao kutumia,
Katika hii dunia, ndio wanaendelea,
Watumwa waliokua, nyuma wanafuatia,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Mifano nakutolea, tokea Australia,
Wezi waliotimuliwa, bara wakahamishiwa,
Waingereza wakiwa, lugha wakaichukua,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Wazungu waliojaa, hapo chini Azania,
Kiingereza kufaa, lugha yao ilikuwa,
Afrikaans kuua, ukuu wakauchukua,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Hakuna palipobakia, sasa panaendelea,
Kwa lugha kuitumia, Kiingereza ilokuwa,
Itazame Nigeria, nayo Cameroun pia,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Unaijua Gambia, na vinavyowatokea,
Uganda na Kenya pia, nadhani wajititimua,
Ila kweli kwendelea, hilo sintatarajia,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Ghana wanajikakamua, mila zinawalemea,
Angalia Ethiopia, nao wanachanganyikiwa,
Na hivi sasa Somalia, nani atakujahamia?
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Afrika kulaaniwa, vya watu kung'ang'ania,
Vyake imeshajitupia, yabaki kujiokotea,
Haina lililokuwa, wala ililolijua,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Viongozi wanunuliwa, lugha ngeni kutumia,
Watu wao ukijua, ni ndogo asilimia,
Lugha wanaoijua, vipi wataendelea?
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Mizizi inatakiwa, maarifa nayo kua,
Hayawezi kuotea, chini isipochimbiwa,
Hunyauka na kuvia, nchi ikasinyaa,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Mbegu nimewaachia, kupanda mnatakiwa,
Viongozi mkipewa, macho waliofungua,
Uamuzi wa kufaa, nchi wakaamulia,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!

Miaka hamtakaa, ndege yenu itapaa,
Mtabaki kushangaa, kwanini mlichelewa,
Kumbe lugha kutokua, ni sababu ilokua,
Siri ya maendeleo, Kiswahili kutumia!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: