Thursday, June 28, 2012

Wahuni wakitawala



Inafaa kulijua, hali inapotokea,
Usalama 'kitumiwa, raia kugeukia,
Mbali hatutafikia, mabavu yatatuua,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Mnyama akiachiwa, damu akajilambia,
Utamu atanogewa, kila sikukurarua,
Nawe hukugeukia,  ndugu pia na jamaa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Huua demokrasia, unazi ukauzua,
Ufashisti kuzua, na watu kuwabagua,
Siasa zikaingia, maendeleo kuvia,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Haki watazichumbua, na uhuni kuutia,
Vipigo vikaingia, na sumu watu kupewa,
Tindikali kutumiwa, usoni wakamwagiwa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Uchu ulivyowajaa, rahisi sana kuua,
Ila kwa yao tamaa, waweze kujipatia,
Hayo wanayofikiria, uungu wakaujua,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Uwizi wataingia, vya watu wakachukua,
Na vilema kututia, hatia tusiokuwa,
Nami ninavyowajua, hapo hawataishia,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Njiani wataingia, kuziteka motokaa,
Porini wakakutia, kisha ukasulubiwa,
Huko wakakuachia, kufa au kujiokoa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Makwenu wataingia, vioja kuwafanzia,
Ni wahuni kwa kuzawa, na pia kwa kutumiwa,
Mungu wamemkimbia, sanamu kujiumbia,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Iko njiani Syria, wahuni mkiachia,
Nchi wataibomoa, kwa kushoto na kulia,
Wakawasagwa raia, kama ng'ombe vile kuwa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Silaha watatumia, raia wakawaua,
Na kisha kusingizia, magaidi wamekuwa,
Na juu wachekelea, wasiwasi kutokuwa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Ni watu waliolaniwa, iblisi awajua,
Kamba amewaachia, wenyewe kujinyongea,
Lakini kujitambua, sio waliojaliwa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Syria yatungojea, kama hivi yanakua,
Polepole hutokea, raia kuhujumiwa,
Kwa vyombo kutumia, wakubwa tu kuwafaa,
Wahuni wakitawala, Syria iko njiani!

Mmea huu ng'oeni



MMEA huu ng'oeni, mtakuwa mashakani,
Mmea wa mumiani, na wauaji wa imani,
Haki wasioamini, na usawa wahaini,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Huwatumia afkani, walojaa kisirani,
Wakawaua amini, wabia wetu nchini,
Ya kwao kuwa yakini, ili wapande thamani,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Mungiki ni wahisani, wameingia nchini,
Wawafundisha uhuni, watu wa chama fulani,
Na wengine serikalini, nao pia wazaini,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Wanafikiri uhuni, waweza leta imani,
Na sheria za hisani, njiani wanabaini,
Haki zisizobaini, binadamu duniani,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Tutafika mahakamani, tuutete walakini,
Mabingwa wenye yakini, wakajaa kizimbani,
Wayaseme ya ubani, sio uongo nuksani,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Nchi hii mashkani, mageuzi tubaini,
Haufai usukani, udhaifu umewini,
Na nchi i mashakani, akibakia kitini,
Mmea huu ng'oeni, kabla haujakuwa!

Polisi bila digrii



Wasiyonayo digrii, upolisi hawafai,
Hawatajua jinai, na katiba kujiwahi,
Mamluki huwatii, sheria wasiitwii,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

La saba twawakinai, jeshi wanalikebehi,
Na dharau ya uhai, kwao yawa usanii,
Hakika hawatufai, kwa katiba hii rai,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Washeheni wanoswii, tena kwa nyingi digrii,
Hawa tukiwastahi, jeshi litakuwa hai,
Siasa litakinai, ustadi wakawahi,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Kusoma wasiojua, wakubwa wawatumia,
Kama maboi wakawa, hadi nyumbani kukaa,
Kila kitu wakapewa, wakubwa kuwafanyia,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Ni maboi wanakuwa, majumbani kutumiwa,
Vijakazi nao pia, nyumbani kuwapikia,
Uoga ukawajaa, haki kutoitambua,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Haki wanaoijua, mambo haya hukataa,
Yao wakayaamua, ya nchi yenye kufaa,
Na uongo kukataa, na watu kuwahofia,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Akili hutumia, si ujinga  kuuoa,
Daraja kujipandia, haki ikitambuliwa,
Na kisomo juu kuwa, ikawajua dunia,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Mahakama zazuliwa, Ulaya kuangalia,
Watu wanaosumbua, kule watahukumiwa,
Nchi haitawatetea, wala wakuu walokuwa,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Wenyewe mnatakiwa, vijana kuyakataa,
Wakubwa kutowatumia, watu kwenda kuwaua,
Dhambi mnaichukua, ni vipi mtajiokoa,
Polisi bila digrii, ni watumwa watakuwa !

Hamuwezi jiokoa, motoni mtaingia,
Unguja hili tambua, na nyie wa bara pia,
Ujinga ukiamriwa, huo lazima kukataa,
Polisi bila digrii, hivi leo hawafai !

Jimbo hili jimbo langu




Mchama kachachamaa, jimbo keshalinunua,
Wengine anakataa, kwake wasije ingia,
Macho wakawafumbua, wale aliowahadaa,
Jimbo hili jimbo langu, mwaja kufuata nini ?

Ni lake kang'ang'ania, hataki kuingiliwa,
Uongo akiuzua, pasiwe wa kumuumbua,
Na wizi akitumia, pasiwe wa kutambua,
Jimbo hili jimbo langu, mwaja kufuata nini ?

Uhuru aulilia, kwa udhaifu kuujua,
Bango anashikilia, la binafsi manufaa,
Na koaja ajivalia, la mfalme juha,
Jimbo hili jimbo langu, mwaja kufuata nini ?

Tuna haki ya kuiba



Chama chetu ni ruhusa, kuiba na kubakua,
Leseni tumeshapewa, nani ataka zuia,
Nchi nzima tumejaa, makaburi kuchimbua,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Makaburi kuchimbua, haki za kuizikia,
Na usawa kukataa, sisi pekee tukawa,
Wajinga wawe waliwa, pasiwe wa kuulizia,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Kibali tumeamua, wenyewe tunakitoa,
Nani atayekataa, na mpini twajishikia,
Makali tukiachia, wote nyie mtaumia,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Kuiba tukiamua, saa yote twachukua,
Ni yetu yanshakuwa, serikali jina yawa,
Chama kimeshikilia, nani wa kukikosoa,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Kudanganya ni tabia, yabidi kuendelea,
Wajinga Watanzania,c hama chetu kinajua,
Kijani ikiingia, na njano inafuatia,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Kijani ikiingia, na njano hufuatia,
Wao basi hupagawa, yote wakatuachia,
Dawa yetu yawafaa, hawana wanalojua,
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Kuwapiga ni tabia, na maji kuwamwagiwa,
Pilipili yalojaa, nao wanafurahia,
Aklili zimewalegea, kitu gani wanajua ?
Tuna haki ya kuiba, wengine hawana haki !

Haki yet u kudanganya



Chama chetu ni ruhusa, kuiba na kubakua,
Leseni tumeshapewa, nani ataka zuia,
Nchi nzima tumejaa, makaburi kuchimbua,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Makaburi kuchimbua, haki za kuizikia,
Na usawa kukataa, sisi pekee tukawa,
Wajinga wawe waliwa, pasiwe wa kuulizia,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Kibali tumeamua, wenyewe tunakitoa,
Nani atayekataa, na mpini twajishikia,
Makali tukiachia, wote nyie mtaumia,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Kuiba tukiamua, saa yote twachukua,
Ni yetu yanshakuwa, serikali jina yawa,
Chama kimeshikilia, nani wa kukikosoa,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Kudanganya ni tabia, yabidi kuendelea,
Wajinga Watanzania,c hama chetu kinajua,
Kijani ikiingia, na njano inafuatia,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Kijani ikiingia, na njano hufuatia,
Wao basi hupagawa, yote wakatuachia,
Dawa yetu yawafaa, hawana wanalojua,
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Kuwapiga ni tabia, na maji kuwamwagiwa,
Pilipili yalojaa, nao wanafurahia,
Aklili zimewalegea, kitu gani wanajua ?
Haki yetu kudanganya, wengine hawana haki !

Haki yetu kuwapiga



Chama chetu ni ruhusa, kuiba na kubakua,
Leseni tumeshapewa, nani ataka zuia,
Nchi nzima tumejaa, makaburi kuchimbua,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Makaburi kuchimbua, haki za kuizikia,
Na usawa kukataa, sisi pekee tukawa,
Wajinga wawe waliwa, pasiwe wa kuulizia,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Kibali tumeamua, wenyewe tunakitoa,
Nani atayekataa, na mpini twajishikia,
Makali tukiachia, wote nyie mtaumia,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Kuiba tukiamua, saa yote twachukua,
Ni yetu yanshakuwa, serikali jina yawa,
Chama kimeshikilia, nani wa kukikosoa,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Kudanganya ni tabia, yabidi kuendelea,
Wajinga Watanzania,c hama chetu kinajua,
Kijani ikiingia, na njano inafuatia,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Kijani ikiingia, na njano hufuatia,
Wao basi hupagawa, yote wakatuachia,
Dawa yetu yawafaa, hawana wanalojua,
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Kuwapiga ni tabia, na maji kuwamwagiwa,
Pilipili yalojaa, nao wanafurahia,
Aklili zimewalegea, kitu gani wanajua ?
Haki yetu kuwapiga, nyie hamnayo haki !

Wasanii watakiwa



Wengine hawatufai, twataka wenye sanaa,
Waitwao wasanii, ajira wakapatiwa,
Hadi ubunge kupewa, kuigiza kwa ridhaa,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Haya ni yetu madai, rahisi twajiuzia,
Shazia pia na sui, sasa twajitafutia,
Huku tunapiga nai, mamluki kuchukua,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Ni chama cha kitalii, hakina kinapotulia,
Huziwamba zake rai, ngoma ikajipigia,
Wetu si wa baibui, nusu uchi wanakaa,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Ihsani hawajui, kidogo kinawanunua,
Na wazee si nishai, bei poa twachukua,
Ni sadaka ya jamii, hili tumeshajaliwa,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Hapana istizahi, wala wa kuwatania,
Hapajawa makuruhi, hishma kuichafua,
Hii ya haki bei, watu tunaponunua,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Kazi yao usanii, kuiga na kuingia,
Kwetu kama makarai, maji budi kuyatia,
Bafuni kuleta uhai, pale tunapojiogea,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Watakiwa wasanii, chamani kuja ingia,
Wakaigiza futuhi, bungeni wakijakaa,
Wananchi kufurahi, wakasahau udhia,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Kama nazi nalo tui, hudamka kitumbua,
Juu ukitia chai, staftahi itakuwa,
Na andazi sikinai, na urojo nao pia,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Watu hawawatambuia, na yao yanayowafaa,
Na pale wanapozirai, wadhani wawazimia,
Na makwetuhawakai, vipi yetu kuyajua ?
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Yawanogea tivii, na sura kujionea,
Hata wasipo na rai, upuuzi kuongea,
Inawatia nishai, nje wakiongelewa,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Vidonda hawaondoi, daima huviachilia,
Sasa inarudi ndui, sanaa yaendelea,
Na ukimwi wajiwahi, fedha wajipukuchulia,
Wasanii watakiwa, kujiunga nacho chama !

Maji yako mgongoni



Ajabu inatokea, hapa kwetu duniani,
Kifuani waingia, kusaka ya mgongoni,
Na kofia wazivua, na nikahi  kuzitoa ?
Maji yako mgongoni, watafuta kifuani ?

Mgongoni yametua, watafuta kifuani,
Ukweli waukataa, na akili hatiani,
Viroja wanvizua, muhali wakabaini,
Maji yako mgongoni, watafuta kifuani ?

Washindwa angalia, Mbelgiji kafanzani,
Na Aishi nakujua, hoteli ya Machameni,
Mashine imetulia, ibura iwafnzieni,
Maji yako mgongoni, watafuta kifuani ?

Mbowe hili alijua, mashine ni ya zamani,
Maji inayaibua, tokea huko bondeni,
Juu yakayanyua, na kwingia hotelini,
Maji yako mgongoni, watafuta kifuani ?

Maji moa yaufaa, Tabora ni Tanganyikani,
Mengine hayo sanaa, tena mkubwa utani,
Mgongoni kunyanyua, yataingia mtaani,
Maji yako mgongoni, watafuta kifuani ?

Monday, June 18, 2012

U a d i l i f u t w a j u a

 
Kuna vyama Tanzania, vya watu vyawaibia,
Ndarahima kunyakua, eti zao kujitia,
Kisha wanatumwaiya, wapate kututumia,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Benki kuu hupakua, mfukoni wakatia,
Watu njaa wakilia, makombo wanagawiwa,
Hazina yapakuliwa, sahani safi zikawa,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Chama kimeingilia, ya serikali kutwaa,
Tumboni wakafukia, vyingi vya kuvibangua,
Nchi mifupa ikawa, yatisha ikitembea,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Ndio wanaviopoa, vya umma vilivyokuwa,
Wao wakajidhania, ndio nchi wamekuwa,
Hofu hawajaijua, umma kuwashtakia,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Ni wizi tunaujua, jingine haliwezi kuwa,
Yafaa kuwaambia, dhuluma wameingia,
Na nchi sasa yalia, wao hawajasikia?
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Na nchi sasa yalia, wao hawajasikia?
Yao yananyakuliwa, hali wanaangalia,
Na waliowategemea, imani imepotea,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Nchi inabakuliwa, na waliodhaminiwa,
Viongozi wananywea, hawataki kusikia,
Miaka yajiishia, na mengi yanapotea,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Na sasa wametokea, wizi wanaokataa,
Ufakiri waujua, walivyo Watanzania,
Kweli wanawaambia, mfukoni wanapwaya,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Michango wajiombea, wanachama kuitoa,
Na pia wote raia, dhuluma wanaokataa,
Ije demokrasia, iokoke Tanzania,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Watu wawanyenyekea, yao kutokuwaibia,
Jasho lao wakatoa, halali kukichukua,
Chama kujijengea, kisafi kilichokuwa,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Wengine wanatumia, kuwakusanya jamaa,
Na kisha wakajitia, wanachama waingia,
Vibaka na changudoa, hadi ndani wamejaa,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Hali kimeshazidiwa, kutapatapa kwamea,
Hakiwezi chini kaa, mikakati kuizua,
Nyadhifa waliopewa, giza mbele imekua,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Miradi wamefulia, upya wafikiria,
Uchama umechachua, hata vipya vyaugua,
Watuwe wameishiwa, mawazo wayadokoa,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Kila mwenye kubagua, vyote akavichukua,
Huja akafilisiwa, akose lilo jipya,
Yake yote huja via, akaanza kulemaa,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Dhulumati walokuwa, laana huwatambaa,
Ikizidi kuingia, huwa wachanganyikiwa,
Ndiyo yanayoteokea, mwisho hatujaujua,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Usiache kuchukua, kitu wakikupatia,
Kisha sadaka kutoa, chama safi kupatia,
Zimwi likawarudia, nje waliloachia,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Kisha kura kuitumia, kwa wasafi walokuwa,
Wachafu wakafulia, kwenye jalala kwingia,
Ndiyo yanayowafaa, kwenye mpya Tanzania,
Huwa wanaviopoa, kisha watu kugawia,
Nasi tumewaelewa, kutuomba kuchangia:
Uadillifu twaujua !

Uadilifu twajua, kumbukumbu yabakia !

Hongereni Chama



Asante chama tawala, kwa vilabu na malaya,
Tabata ni halahala, sasa hivi twavamiwa,
Kama hutaki kulala, njoo vingine potea,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile Kinondoni,
Kwa pombe na Changudoa !

Tumefanyiwa fadhila, kuenezewa mabaa,
Hii sio kama lila, ni yetu njema hidaya,
Tunaliwa, tunakula, wala hakuna umbeya,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile ni Ohio,
Kwa pombe na Changudoa !

Kata yetu ni jalala, kila kitu twatupiwa,
Tumezawadiwa  hila, ili kizazi kuvia,
Unajua utawala, kibali waliotoa,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile Kinondoni,
Kwa pombe na Changudoa !

Wengine juu walala, chamani wametulia,
Na kura wameshakula, japo kwa kutuibia,
Wakishazipata hela, nasi hatutawafukia,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile ni Ohio,
Kwa pombe na Changudoa !

Wajifie kama swala, porini walikokuwa,
Funza wapate kuwala, mchangani kuishilia,
Hiyiondiyo yetu sala, nyingine hatutaijua,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile Kinondoni,
Kwa pombe na Changudoa !

Kwa kweli ni kama swila, watu hawa nawambia,
Simu yao ina dola, hakuna wasilojua,
Kuua kwao ni mila, ukwasi  kuufatia,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile ni Ohio,
Kwa pombe na Changudoa !

Katuambia Makilla, mtunzi alojaliwa,
Mola amtunze Mashallah, kwa ukweli kuutoa,
Ajua bila jamala, italia Tanzania,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile Kinondoni,
Kwa pombe na Changudoa !

Haya ndio masuala, watunzi kuzungumzia,
Kajitoeni kafala, haya kuyasabiia,
Kafiri wana madhila, imani zatupotea,
Hongereni chama hiki, kwa kuifanya Tabata,
Kama vile ni Ohio,
Kwa pombe na Changudoa !



Ushoga kukaribia


Ni ugonjwa wa tabia, za ukwasi na kinaya,
Wale waliojaliwa, baraka kuichukia,
Na halali kilokuwa, wakawa wakikataa,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Haramu hutamkia, ndicho huchangamkia,
Nani wa kumsikia, si adhana wa kutia,
Wala mnadi swalaa, na maji wa kuchotea,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Sikio vigumu dawa, kuweza kuiskia,
Bure utaliumbua, uziwi ukaingia,
Vyema ni kuyaambaa, na mbali sana kukaa,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Kizazi kikiujua, kitataka kurejea,
Ni mafunzo yatolewa, ole wanayoendea,
Mwana usiyemlea, chochote aweza kuwa,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Tusiifate dunia, wana wakatupotea,
Vyema kujiangalia, na rafiki kuchagua,
Watu mkiwavamia, mtakuja jijutia,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Subira inatakiwa, na mwendo kuangalia,
Tusitwae lawalawa, roho tukaziachia,
Na wanaonisikia, ushahidi nimetoa,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Na wanaoyaachia, wengi wao twawajua,
Madawa walianzia, sasa ushoga watia,
Kesho hatutaijua, pengine waje kuua,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !

Ninamuomba Jalia, haya kutuepushia,
Isije kuwa balaa, juu jengine balaa,
Nchi ikalaaniwa, na vizazi kufatia,
Ushoga kukaribia, waweza kukuathiri !


Mchezo wa kuigiza



Ukweli tukiujua, watu wema tungekuwa,
Ni mafupi yalokuwa, maisha kwenye dunia,
Siku kasi hupotea, na wewe ukapotea,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Ni mchezo ulokuwa, watu tunajichezea,
Makubwa 'kifikiria, kichwa bure waumia,
Muda hautakawia, watalishusha pazia,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Ukubwa huulilia, hadi ukajipatia,
Madudu ukaachia, watu wote kukuchukia,
Kisha hubaki walia, nafasi tena  kupewa,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Watu wanjisomea, shahada wakazitwaa,
Wengine bure wapewa, tena wanachekelea,
Kitu hawakutumia, na uchungu hawatojua,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Mwenye elimu huvia, na yake yakapwelea,
Pasiwe kusaidiwa, japo keshasaidia,
Na pembeni hutupiwa, kcihwani kujiozea,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Wazuri wanazaliwa, bahata wakachezea,
Wakija kujitambua, umri wakomalia,
Wakabaki jichubua, kumbe ndio wajiua,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Mamissi waliokuwa, uzee huja ingia,
Watu wakawakimbia, uzuri waliojaliwa,
Wengine wakaridhia, mapenzi kuyanunua,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Wachamungu huishiwa, watu wakawanunua,
Mfukoni kuwatia, yao wakakubalia,
Ghafla hushtukia, sakramauti yatua,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Nani atawaombea, waliokwishalaaniwa,
Kufuru waliotia, na Mola kumchezea,
Utani huwarudia, na shiriki kushtakiwa,
Maisha tunayoishi, mchezo wa kuigiza:
Tunapanda jukwaani,
Kwa muda ni wasanii,
Kisha chini tunashuka,
Na kupotelea mbali!

Miongoni mwa fisadi


WAKOLONI wamekuwa, nchi tuliowaachia,
Yalayale yalokuwa, ndio wameyakamia,
Ni kuganga yao njaa, na nchi  kuachilia,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mkoloni amekuwa, mweusi aliyekuwa,
Mweupe kawaachia, nao wanayatumia,
Huu mkubwa udhia, pale wanaponunuliwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Kila kona natembea,  hata chini kufukua,
Chama sijashuhudia, cha wazawa kubakia,
Vyama vimenunuliwa, na tajiri mujiria,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Watu vinawaibia, kwa kushoto na kulia,
Hazina wazivamia, na cha watu kuondoa,
Na kodi wakichukua, wajua wanavyotumia,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mishahara wanyanyua, waheshimiwa kung'aa,
Matumbo wanajazia, hakuna cha kupungua,
Huku watu wafa njaa, na bei juu zapaa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Neema wajigawia, mfukoni wakatia,
Mali kujilimbikizia, bilauri zimejaa,
Sasa wanajimwagia, wenyewe kujichafua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Fisadi wameingia, hazina wanabomoa,
Kilichomo kuchukua, vyama kwenda kuvifaa,
Kidogo huvipatia, kingi wao kuchukua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Dala tunaisikia, na dola twaitambua,
Milango walofungua, mbona wote twawajua,
Hazina wakaachia, kilichomo kuibiwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Akili watuchezea, kwaa vijisenti kupewa,
Fikra wameishiwa, ujanja wanatumia,
Uongo sasa wazaa, na ni kazi yao kuulea,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Dhahabu wameachia, wazungu waichukua,
Na ajabu ilokuwa, ni pipi walipokea,
Kila mtu ashangaa, muflisi tumekuwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Miradi wakiandaa, ni pasenti kupatiwa,
Tena mingi imejaa, mingi yajaa udhia,
Kazi kubwa kutwibia, ili wao kutumbua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mazao yanapotea, na kilimo chafifia,
Hawa ukiwafatia, mwisho mbaya watujia,
Na linalotakiwa, mikakati kuamua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Maradhi yanaenea, kama mwanzo kuanzia,
Watoto wanajifia, kwashakoo kuvamia,
Na bongo zinafifia, elimu yawakataa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Elimu wanaiua, na ushindani kupwaya,
Kila kitu twanunua, toka kwa waliojaliwa,
Sisi soko tumekua, kila kitu kutupiwa,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Mikakati walozua, masikini wazidia,
Badala ya kupungua, hivi sasa waenea,
Maana wanaojifaa, ni wenyewe wajijua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?

Uzalendo waniishia, kwa uongo kukataa,
Hawa wanaoututania, sidhani wanajijua,
Kazi kwao itakuwa, wakija kujitambua,
Nani mwenye uzalendo, miongoni mwa fisadi ?


Mikoa mingine mikubwa kuliko nchi ....


TUME ninaiambia, kuna pande yaonewa,
Na hivyo mlivyokaa, haya yote mwayajua,
Kuna mingine mikoa,  zaidi ya nchi huwa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Na mikoa kwendelea,
Ushindani ukakua
Ikomboke Tanzania!

Mikoa inatakiwa, viongozi kuchagua,
Si wa kuteuliwa, zawadi wanaopewa,
Kuwajibika ikawa, kitu wazi kilokuwa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Viongozi kuchagua,
Kusimamia mikoa,
Huru ikawa mikoa.

Haki zao walilia, watu kwenye mikoa,
Serikali kuu mbia, ndio iwe na mikoa,
Yenyewe kutoamua, yanayohusu mkoa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Mikoa kutovamia,
Rasilimali kutowa
Wazawa wakawa sawa!

Mbalimbali itakuwa, kiutawala mikoa,
Ila ni kimoja twawa, shirikisho kutulea,
Pasiwe wa kuonewa, wala wa kupendelewa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Shirikisho kuwa dawa,
Haki kuziangalia,
Mkoa kutojichafua !

Vyuo vikuu kuzua, wana wakajisomea,
Na si kujipendelea, wakubwa wlaiokuwa,
Ni haki kila mkoa, chuo kujijengea,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Chuo Kikuu kuzua,
Iwe hadhi ya mkoa,
Na yao kuangalia.

Waziri mkuu akiwa, haki ataangalia,
Mkoa kuutetea, mamboye kufanikiwa,
Nchi jirani zikawa, uchumi zinachangia,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Waziri Mkuu akawa,
Asimamia mkoa,
Wakazi wamemchagua!

Shule watazipanua, kimataifa zikawa,
Wanafunzi wakajaa, nchi jirani watokea,
Elimu kufurahia, hadhi juu imekuwa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Mawaziri wa mkoa,
Wawe wamsaidia,
Mkoa haraka kukua.

Hospitali kung'aa, huduma zinazofaa,
Tele vikawa vifaa, kupima na kutibia,
Nje wanaotibiwa, hapa kwetu kupokelewa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Mawaziri wa mkoa,
Wawe wamsaidia,
Mkoa haraka kukua.

Huko ni kuendelea, si ngonjera kutia,
Kufumba na kufumbua, hutoijua Tanzania,
Ni nyingine itakuwa, daraja kujiipandia,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Mawaziri wa mkoa,
Wawe wamsaidia,
Mkoa haraka kukua.


Bunge litalozaliwa, la  mkoa litakuwa,
Muda kidogo kongea, mwingi ni kutumikia,
Vijijini kuingia, matatizo kutatua,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Pawe na bunge la mkoa,
Maendeleo lalea,
'Wakilishi maridhia.

Wajumbe wake wakawa, maslahi watetea,
Makundi yote ya mkoa, uwakilishi wakawa,
Na yao kuangaliwa, daima yahifadhiwa,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Pawe na bunge la mkoa,
Maendeleo lalea,
'Wakilishi maridhia.

Wakulima kuingia, wafanyakazi nao pia,
Wakwezi wakaenea, mipando kuzungumzia,
Hata pia injinia, na madaktari radhia,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Hawa hawatasinzia,
Kuitetea mikoa,
Fani zao watokea,
Ya kwao wapigania.

Mamlaka twatakiwa, katiba iliamua,
Mikoani kuingia, wakazi wakachukua,
Leo twang'ang'ania, aibu tunajitia,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Kutonyonga vyakukua,
Nchi kubwa twaijua,
Dar mbali yasogea !

Atuongoze Jalia, marhaba yetu kuwa,
Tuijenga Tanzania, mpya iliyokuwa,
Na vizazi kushanga, akili tulivyotumia,
Hadhi sawa ikipewa, mikoa na Zanzibar:
Ndio haki itakuwa,
Hivi hamjakujua,
Dunia yaelekea
Nchi ndogo kuzaliwa,
Na kubwa zikajifia !!!



Moja, mbili ya kichanga



NI ajabu ilokuwa, hii yetu Tanzania,
Hufa na kufufuliwa, za chama zilozokuwa,
Kale wakaifukia, na upya wakaanzia,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Rojo sana imekuwa, serikali Tanzania,
Maji yanaizidia, siasa zilizojaa,
Na haliwi la kukua, lawama zaendelea,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Kutengwa inatakiwa, ya serikali yakawa,
Chama mbali yake kuwa, utawala kuachia,
Vinginevyo kama yawa, mwisho watayajutia,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Katikati huishia, kila linalobuniwa,
Rais mpya akawa, ya kale yasahauliwa,
Mapya akaanzia, na kichwa yasiyokuwa,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Sanaa twajionea, sinema isiyofaa,
Kwa wengi kizaazaa, na nusura waijua,
Mambo yanavyojiendea, kama 'sukani watoa,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Kama meli ingekuwa, kuzama ingeshakuwa,
Bali vizibo vyatiwa, tungali tunaelea,
Ukubwa ukilemaa, nchi nayo hulemaa,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Hadhi juu ingekuwa, hii yetu Tanzania,
Nuksi tunajitia, kwa kujifanya tunajua,
Vilo bora twafumua, na ovyo kujishonea,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Mikakati yatuumbua, kipi kipya kimekuwa,
Zama yaljaribiwa, na bado tukapotea,
Na mikono yaungua, jikoni tukiingia,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

Atunusuru Jalia, watuwe kutwangalia,
Uoza kuukimbia, kwa harufu na kinyaa,
Upya tukazaliwa, usafi 'kishadidia,
Serikali zetu hufa, na kisha zikafufuka:
Upya tena kuanza,
Moja, mbili ya kichanga !

T A N G A N Y I K A, T A N G A N Y I K A



WASOTAKA Tanganyika, yao wameshaamua,
Wayasema kwa mashaka, busara hawajajua,
Msiba utatufika, hilo lao kijakuwa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Usanii wafanzika, uchama kuuridhia,
La umma kukatalika, azma yao ikawa,
Na Mola alimulika, hili ni vigumu kuwa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Nchi zilizoungika, kitu kimoja kikawa,
Mzizi unaoshika, nchi mbili hutambua,
Ya tatu ikafanzika, ubia kuchaguliwa,
Mkiua Tanganyika, muungano utapona ?
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Leo tumeathirika, moja imezainiwa,
Na watu wanapotaka, mizengwe wanafanyiwa,
Haudumu ushirika, usawa usiokuwa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Kwa watu yahitajika, haki kuizingatia,
Na eneo kadhalika, kwa ukubwa kuridhia,
Na jambo likifanyika, adili yazingatiwa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Nawajuza wasifika, mbele yatakayotokea,
Tanganyika mkizika, Tanzania mwaiua,
Moyoni sina mashaka, hili budi kuwafika,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Wapo waliotukuka, haya waliyakaa,
Na siku ilipofika, wote wameadhirika,
Urussi yalifanyika, leo tunajionea,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Kwa Tito mstahika, yalijiri Yugolavia,
Mauaji kufanyika, na udini kuuzua,
Bure mnahangaika, moto petroli mwatia,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Msingi haujajengeka, kuta mnakimbilia,
Nondo hamjaziweka, nguzo mnang'ang'ania,
Ni ajabu kuinjika, chungu bila ya mkaa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Funguo tumezishika, katiba kuifungua,
Tuzungumze hakika,na kinani kuingia,
Ikibidi kufumuka, hayo yetu maljaliwa,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?

Tuyaondoe mashaka, vichwa vyetu kutulia,
Tuwe nayo ya hakika, yaafayo zungumzia,
Midomo ikifungika, uzaini twautia,
Tanganyika, Tanganyika, hivi nani kaiua ?


Chama ana malaria ?

KAMA chama chaugua, hivi nini inakuwa,
Ugonjwa ukaujua, eti tena malaria,
Chandalua kimevaa, wapi mbu kaingia ?
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Kauli za kuugua, kila siku zatokea,
Huzuka kwenye mitaa. pia kwenye majukwaa,
Kichwani yameingia, yasemwayo hushangaa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Chama kinajitambua, uchama kikalilia,
Kisha huchanganyikiwa, uchama kikakataa,
Halafu kikakwambia, serikali kimekua,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Huvaa hii kofia, mengi kikayaongea,
Na ilani zisokuwa, uchama kinachofaa,
Si kwa nchi kutumiwa, wala watu kuwafaa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Na mwili ukipungua, watu hukiangalia,
Mengine wakadhania, kukonda ilivyokuwa,
Hungong'ona nje wakiwa, eti kimeshaukwaa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Dawa kinapotumia, malaria kuondoa,
Afya hukirudia, ila akili nazaa,
Pia ungali umbeya, eti dawa zinakifaa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Ukimwi naukataa, jama haya malaria,
Kichwani yameingia, ndiyo tunayojionea,
Waganga hawataa, hospitali twatakiwa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Chama anaugulia, huku na huku ahaha,
Ugonjwa hajaujua, kulogwa anahofia,
Huyu ni wetu jamaa, ukweli sikumwambia ?
Chama kina malaria, au huu ni ukimwi ?

Kumuuguza inafaa, presha ikapungua,
Amana tumeachiwa, lazima kumwangalia,
Akija kutufilia, sisi tutalaumiwa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Kichwani inapokaa, mbaya kweli malaria,
Mtu huwa kama kichaa, vituko akavizua,
Njiani akakimbia, ikawa kubwa balaa,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?

Yatakiwa kumzuia, asigongwe na motokaa,
Hadharani kujifia, watu wanamwangalia,
Huruma imeshapotea, watu weza jipitia,
Chama ana malaria, au huu ni ukimwi ?


Watu mengi wanaweza


Hawawezi viongozi, watu wetu wanaweza,
Songea ona uzuzi, lao wameshatangaza,
Akili tukdarizi, budi hawa kuwatunza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Walakini uongozi, watu unaolemaza,
Changamto hawajuzi, watu wenywe kufanza,
Watuona vijakazi, mzungu  tu anaweza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Matatizo hayawezi, watu yakatuongoza,
Ama  huo upuuzi, hili ninalitangaza,
Kama wao hawawezi, mbona sisi tunaweza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Palipo na utatizi, wakazi kujiagiza,
Nini hatukiwezi, na lipi tunaloweza,
Tukafanza upanguzi, na mikakati kujuza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Wamelala viongozi, wadhani hatutaweza,
Kitu hawatuagizi, wadai sio wafanza,
Huu kwetu uchochezi, Songea wameshatujuza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Uongozi utatuzi, ndio kazi ya kufanza,
Ofisini mkibarizi, hivi lipi tutaweza,
Shukeni kw ahizo ngazi, vitendo kuvisambaza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Watutoka usingizi, watu sasa tuanweza,
Tukiongeza ujuzi, hata ndege kutengeza,
Pasiwe na vizuizi, kwa mis'ada tukaoza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Kitaifa hamuwezi, mtaziidi tuuguza,
Kwendelea h atuwezi, kwa misaada kutuponza,
Tujishushe wenye enzi, yetu yote kuyafanza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Yaleta heshima wazi, kila mtu anajuza,
Na hao wa nje wezi, wakaacha tuchuuza,
Kwa akili na ujuzi, tukawa yote twaweza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Wakowapi viongozi,  hili wanaloliweza,
Kuyafanza mapinduzi, tuachane na kuoza,
Mzungu kama mjuzi, h awezi kutuendeleza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Tutangaze mageuzi, kuwa nchi inaweza,
Na mikoa ufunguzi, kwao wanayoyaweza,
Ruvuma mkubwa mjuzi, mfano keshatangaza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !

Tusiseme hatuwezi, Mola tutamchukiza,
Akili keshatuenzi, kuzitumia twaweza,
Hii leo sio juzi, nchi kuitengeneza,
Watu mengi wanaweza, kikwazo ni viongozi !


Ufukara wa kutisha

Kufilisika si kwema, kuwe kwa kila aina,
Ila ni kubwa nakama, ukiwa ni kwongozana,
Ikawa mwarudi nyuma, kwenda mbele mnaona,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Watu hukosa ujima, pasiwe nala kusana,
Mbingu zikawa zahama,  na dhiki zawatafuna,
Pasiwe mwenye kusema, lililojaa maana,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Nchi ikiwa yatima, kwa viongozi haina,
Haina inachosema, wala kuweka amana,
Na haishi kuazima na wengine kukopana,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Hulemaa wakazama, viongozi wakanuna,
Pasiwe yenye adhima, wawezayo kuyafanya,
Lakini wanarindima, kwa kung'aa na kunona,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Ufukara huu ngoma, kuicheza patasuna,
Zinatoweka hekima, ikabakia kuguna,
Na busara huroroma, usingizini kutuna,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Akili huwa zagoma, hata vichwa ukikuuna,
Kisogo ukakitoma, na ukuta kugusana,
Giza likawa latoma, na kitu kutokiona,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Hubakia vicherema, vichuguu hutonena,
Pasi nuru ya kalima, vilimo kutoviona,
Wakaingia songoma, yao wakaja kuvuna,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Naye siye maamuma, ayajua maulana,
Hamuwezi pewa chema, msio na muamana,
Mtapewa chenu kima,  hadi kuwa waungwana,
Ufukara wa kutisha, ni ule wa uongozi !

Usanii unakwisha



Ukikoma uigizaji, utaisha usanii,
Mvua ikiwa maji, hewa haifikirii,
Wajinga na wajuaji, ndoa yao haikai,
Uigizaji ukikoma, usanii utaisha !

Mlaji sio mkaji, yake huwa hayakui,
Fundi hamzidi gwiji, ndoo yake haijai,
Hauwezi kunywa uji, ikawa sawa na chai,
Uigizaji ukikoma, usanii utaisha !

Si mtenzi mwigizaji, ndo maana hafulii,
Wa kinywaji na kilaji, tui wala halijui,
Usimpe mfamaji, mkono hauachii,
Uigizaji ukikoma, usanii utaisha !

Kadhalika mshukaji, kwa mkono humsalimii,
Kama wewe mpandaji, awweza kunanihii,
Na daraja sitaraji, siri zangu siachii,
Uigizaji ukikoma, usanii utaisha !


Watu ni sisi wenyewe



Chetu ni nani kavaa, kiatu tulichopewa,
Atakiwa kukivua, wenyewe tukakivaa,
Sivyo atatuchezea, na uhuni kutufanyia,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Katiba yatuambia, ndivyo ninavyotambua,
Madaraka tumepewa, na mamlaka kujaliwa,
Nchi kuisimamia, kwa umoja wetu tukiwa,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Kazi tunaowaachia, ukubwa si kuchukua,
Mabosi tunabakia, hili wapte kujua,
Uongo wakiutia, mara moja kuwatoa,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Uwizi tukisikia, hakuna kuwaachia,
Watu sasa wamejaa, kazi hizo wazijua,
Ofisi waking'ang'ania, ni budi kuwatimua,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Rushwa wakiipokea, au fisadi kuachia,
Pasiwe na kuchelewa, lazima kuwatimua,
Ubosi tuantakiwa, wao wapate tambua,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Katiba inatakiwa, mpya ikitujia,
Hili kulitambua, na mengine kuyazua,
Kinga ikaondolewa, maovu tukifichua,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Kuna vyombo wameua, sisi tunawaachia,
Twazidi kuvumilia, nchi inadidimia,
Haya yasingelikuwa, uwajibikaji ukiwa,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Kuna uongo  watia, hata wanapotambua,
Na ukweli kufukia, ili kufanza hadaa,
Hakika wanatakiwa, watu hawa kutokaa,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Hazina waidonoa, kwenda wao kuwafaa,
Katiba tukifatia, tungekwishaondoa,
Ila bado twapumbaa, mpya kuingojea,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Watu sasa kutmbua, uongozi sio raha,
Yaweza kugeukia, makini usipokuwa,
Ukubwa wenye balaa, watu wanaukataa,
Watu ni sisi wenyewe, kiwapikiatu chetu ?

Alozoea kuomba



Kuomba aliyezoea, huwa ni yake tabia,
Vigumu kuiachia, hiyo nayo kazaliwa,
Nyayo anazifuatia, karunini kusishia,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Hawezi vingine kuwa, hiyo ni yake tabia,
Kayajenga mazoea, kila kitu kutegemea,
Aibu wala si haya, kwake anayoijua,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Kuomba ataringia, na wengine kuvutia,
Akaijenga himaya , yao watu wa kupewa,
Roho zote zikavia, kwa wengihe kutegemea,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Mola hili achukia, viumbe mliojaliwa,
Viungo vikatimia, na akili kuzipewa,
Thamani huwapungua, muwe msiyemfaa,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Viumbe mnatakiwa, jasho lenu kulitoa,
Mlacho kufurahia, kazi mmekifanzia,
Ila hayo ya kupewa, sivyo y anayotokea,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Yaoneni ni kinyaa, muanze kuyakimbia,
Watu wakiwatumia, kwa  nguvu kuyakataa,
Msipokee dagaa, hali mwajua kuvua,
Alozoea kuomba, tabia huendelea!

Aabuduye wageni



Aabuduye wageni, kwao wao si mgeni,
Na mkazi baniani, atamshinda mgeni,
Maisha kitu amini, ukaapo uthamini,
Aabuduye wageni, huwa hanayo mzizi !

Wengi wako mashakani, kwa kuthamini wageni,
Huipiga abautani, mambo mkija wahini,
Dhikini kuwaacheni, mkakosa tumaini,
Aabuduye wageni, huwa hanayo mzizi !

Watawaacha jangwani, hamna matumaini,
Wakarudi masikani, wakuitako nyumbani,
Hali yenu sasa duni, mmebaki makatuni,
Aabuduye wageni, huwa hanayo mzizi !

Huu ni wao uhuni, huufanza duniani,
Hawali nanyi amini, wala msiwaamini,
Ila kiasi hisani, mkawajua moyoni,
Aabuduye wageni, huwa hanayo mzizi !

Wengi wao ni rehani, na riba huwazaini,
Wakaufanza utani, yao mkayathamini,
Njia wakiibani, wakitoka hamuwaoni,
Aabuduye wageni, huwa hanayo mzizi !


Aabuduye Wazungu


Aabuuduye wazungul, hubaki na makamasi,
Akaiona mizungu, na mkubwa wasiwasi,
Asozawa na uchungu, aweje na udamisi ?
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Chungu hakiwi mkungu, na nazi  haiwi nasi,
Lake haliwi ni langu, kwa kidogo na kiasi,
Sijaujua mvungu, urefuwe kinamasi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Ni heri mlaji dengu, choroko sio nuksi,
Watayapanga mafungu, tena pasipo uasi,
Wakaukuza undugu, kwa ndoa nazo harusi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Wazungu watu wa tangu, yetu hawajayaanisi,
Nchi kwao ni mkungu, ndizi wanatanafusi,
Zinapofunuka mbingu, hata nazo huakisi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Ukimfanza ni Mungu, kwake huwa ni rahisi,
Hukufanya ni kijungu, akakutia yabisi,
Akakulisha na kungu, uzidi kuwa mwepesi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Hapa kwetu hana fungu, ila kwao wadamisi,
Wamejitia vifungu, kuifunga kadamasi,
Fungate yenye uchungu, na kuibiwa kwa nafasi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Siyajui ya wenzangu, siyapendi makamasi,
Na mafua ya uchungu,yatiayo wasiwasi,
Ningekimbia wazungu, Wachina kuwadurusi,
Aaabuduye Wazungu, hubaki na makamasi !

Mdharau watu wake



Huidharau mwenywe, mdharau watu wake,
Kiki'sha chake kiwewe, ni ukweli ufumbuke,
Mgeni ni kama mwewe, hutua chake adake,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Mgeni ni kama mwewe, hutua chake adake,
Kwa kasi yake atuwe, papo hapo aondoke,
Kwalo hilo muelewe, si udugu autake,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Kwalo hilo muelewe, si udugu autake,
Hutaka chake azowe, na nyumbani akiweke,
Vipi akufae wewe, yapungue mali yake ?
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Vipi akufae wewe, yapungue mali yake ?
Mlishwao msiwe, wa pipi za mate yake,
Muone mbarikiwe, hatimaye mzuzuke,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Hujidharau mwenyewe, mdharau watu wake,
Huwasemi waelewe, kwalo hilo awajibike,
Hujidhania ngewe, naye siye ahusike,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Siyo hivyo nielewe, hayo si mashiko yake,
Kiongozi mwenye ndwele, huwalaumu wa kwake,
Akabakia mwenywe, nalo lake lisifanzike,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Hujidharau mwenyewe, mdharau watu wake,
Ni nani amuokowe, ikifika siku zake,
Huja yake yaishie, alipo asitukuke,
Mdharau watu wake, hujidharau mwenywe.

Ni vyema kumkataa



Tabia ni mazoea, kuisha haitakuwa,
Fisadi aliyekuwa, kati hawezi achia,
Na kila mwenye kunukia, yafaa kumuambaa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Utamu ukimkolea, pima ataichukua,
Hutaka jiongezea, kikubwa zaidi kuwa,
Pasiwe wa kutangulia, sifa yeye kuchukua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Pasiwe na kupungua, nyuma aje kurejea,
Mbele ndo yake njia, hatotaka kuchelewa,
Pumzi akipumua, huiwazia dunia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Huiwazia dunia, na yake yapate kuwa,
Mipango kutoijua, mingine kuandaliwa,
Alaa akangojea, kumnasa apajua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Uuungu watajitia, na mbwembwe kukumbatia,
Hutoa na wakatwaa, na vya watu kuchukua,
Ni mabwana walokuwa, watwana wasaidia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Huvua wakayavaa, watende na kutendua,
Kaya wakaziingia, na kuzitwaa hidaya,
Wakaonekana poa, kwa misaada kutoa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Mashemeji wa ridhaa, na bandia walokuwa,
Na wana wa kujilia, hata nje huzaliwa,
Na asili kuijua, ngumu sana kuijua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Waganga huwafumbia, giza likawasugua,
Vioo wakakimbia, ukweli vinavyotoa,
Vyoo vyao vikijaa, marashi huongezewa,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Na maua yakatiwa, kwa rangi za kuchagua,
Jasmini ikafaa, mawaridi nayo pia,
Ila zamu hufatia, kunuka na kunukia,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!

Fedha zinawazuzua, njaa inayosumbua,
Sasa wanunuliwa, kukitakasa kinyaa,
Heshima yawapotea, nao hawajajijua,
Kila anayenukia, harufu ya ufisadi:
Ni vyema kumkataa!


Utamsahau ?



KILA mtu awajua, yeye tunamshangaa,
Ushoga kauingia, mchana uliokuwa,
Heri akiitazamia, kwingine 'sikotokea,
Hivi utamsahau,kula naomumiani ?

Na taasisi kadhaa, na wengine kugaia,
Misaada kuitwaa, ili wakajishibia,
Na kila mwenye kujua, zimwi ameshaingia,
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Upofu wamewatia, na uziwi nao pia,
Yamekwisha majaliwa, dhahabu kugnguliwa,
Ndani ameshakaa, kumtoa ataua,
Hivi utamsahau, kula naomumiani ?

Tabasamu kajaliwa, kulemaza na kuua,
Kila nikiangalia, sioni pakutokea,
Na vikosi vyaingia, uhasama kuja zua,
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Safari zilizokuwa, puani kututokea,
Na uongo wakazua, yao kuja kuwafaa,
Marafiki watajaa, maadui walokuwa,
Hivi utamsahau, kula naomumiani ?

Saini wamezitia, ya kwetu kutuibia,
Ni kushoto na kulia, hapana palipobakia,
Mumiani waingia, damu kuja jinyonyea,
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Vya neti wanajilia, vya ukimwi vyafatia,
Uongo na  kweli huwa, yote wanojifanzia,
Salama yao hadaa, kuna yao kutimia,
Hivi utamsahau, kula nao mumiani ?

Tumezizua sheria, watu wetu kuwagawa,
Wakubwa wanunuliwa, haki wanaziachia,
Mfukoni wametiwa, kutoka ninahofia,
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Oneni yanayotokea, kwa pipi mnazopewa,
Dhahabu wanachukua, kila kitu mwaachia,
Ufukara mwajitia, muombe kusaidiwa ?
Hivi utamsahau, kula nao mumiani ?

Huu mkubwa mzaha, masikini Tanzania,
Ombaomba tunakua, utajiri umejaa,
Akili tumelemaa, na watu tunatumiwa?
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Wakubwa tunateua, waliozidiwa njaa,
Makombo wakipatiwa, waona wamejaliwa?
Pasi aibu wala haya, wasema tumeendelea?
Hivi utamsahau, kula nao mumiani ?

Sahau haitakuwa, kumbukumbu zitakaa,
Uhai wakijaliwa, wenyewe kujionea,
Na watu wakaamua, nini cha kuwafanzia,
Hivi utamsahau, kunywa nao chinjachinja ?

Balaa kuiondoa, dua zetu zatakiwa,
Kila siku, kila saa, Mola tuwe twamlilia,
Hupangwa akapangua, naye njia anazijua,
Hivi utamsahau, kula nao mumiani ?

Ukicheza na mbwa



ACHA na mbwa kucheza, asije kukuchezea,
Bila ya kukuuliza, msikitini huingia,
Keshakuona ni mwenza, kucheza ajisikia,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Kuna watu wa kuoza, kazi yao kutumiwa,
Heri hata ya mafunza, wanajua pa kukaa,
Hawa si wa kufunzwa, utu kwao ni kinyaaa,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Akili zao huviza, haki kutoitambua,
Wakayameza ya viza, kutupwa yanayofaa,
Ukweli huwa waiza, wanajali manufaa,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Shere bila kuwacheza, wewe watakuchezea,
Ngoma ukiituliza, na akili kufungua,
Jibari huwamaliza, neno wakalielewa,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Njaa tuu inawauza, si watu wa kujitambua,
Na wakizuka waweza, riziki wakawapatia,
Ya wengine wakaiza, yako wakayasikia,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Na huu si muujiza, ujanja wanaujua,
Upacha wanauteza, huku na huku kufaa,
Na zao lao hukuza, mara mbili kuja kuwa,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Mbwa ukishamfunza, mlinzi huweza kuwa,
Akulinde si kubeza, kazi akajifanzia,
Na wewe ukamtunza, yeye kukuangalia,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Chema kweli chajiuza, hivi nani asojua,
Kibaya chajitembeza, kwa thamani kupungua,
Hata nawe ni muweza, hili waweza tatua,
Ukicheza na mbwa, msikitini huingia !

Sunday, June 17, 2012

Una umuhimu gani kwangu ?


Hali yangu hujajua, wala kuniangalia,
Vipi itatokea, iwe nakutetemekea,
Itakuw ani ngekewa, vigumu kujipatia,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Ni maiti anakuwa, yule asiyenifaa,
Dunia hujiendea, hata nsipomjua,
Yakawa yanayokuwa, si ajabu kuzizua,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Nini umenifanzia, yako wewe kuyajua,
Lipi umelisikia, adhana na kukimiwa,
Moyo ukakushtua, na  kuniombea dua,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Lini tonge umetia, ukawa waniwazia,
Mkononi kusalia, wasiwasi kukujaa,
Hadi ukanipigia, hali  kutaka kujua ?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Kipi umenitendea, niwezacho jivunia,
Nisiache toa dua, mazuri kukuombea ?
Kitandani 'kiingia, shukrani nikatoa ?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Lini umeangaliwa, wangu niliojaliwa,
Hata shauri kutoa, pasina kugharamia,
Ukaelekeza njia, yao nao kutimia ?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Lini umehudhuria, kilio nilichofiwa,
Na ubani kuutoa, kwa siri kujifanzia,
Na sadaka kuitoa, machozi yakapungua?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Siku gani ilikuwa, yako mimi kunifaa,
UKapungua ukiwa, kwa hisia za jamia,
Nami nikajiinamia, na hofu kuiondoa?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Sababu sijaijua, muhimu kwangu ukawa,
Hebu niachie njia, uendako elekea,
Na shari ukiizua, kheri nitakuombea,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Madeni wanilindukia, hayawezi kupungua,
Na riba zanizidia, nazidi kudidimia,
Huruma hukujaliwa, unafanya ya mzaha?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Naona umelaaniwa, ya watu kutosikia,
Kaziyo kushtukia, ukazichora sanaa,
Na mengine ya umbeya, tija yasiyojaliwa,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Viwanda umeviua, na ajira kupotea,
Vijana wakukataa, jahili unshakuwa,
Usiende kwenye mtaa, au utajaumia,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Vijiji vimedumaa, huna aibu wala haya,
Wathubutu kujitoa, kujitia kidedea,
Ni maradhi umekuwa, budi tu kuvumiliwa,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Kilimo kimejifia, na ubani hujatoa,
Watu wanakushangaa, matumizi wazidia,
Badhirifu umekuwa, fisadi wawaachia,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Mikopo unayopewa, njiani inapotea,
Ukadai waibiwa, wezi hujatutajia,
Kidole chakuelekea, hivi hili hujajua ?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Wapika na kupakua, msaada wakataa,
Na wasomi wamjeaa, uchumi wanaojua,
Wajifanza unajua, kumbe huna unalojua?
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?

Bajeti nakuambia, zuri kwako sijajua,
Ninazidi  kuumia, na watoto wasinyaa,
Nenda zako u balaa, wengine nawangojea,
Kama hunifanzii kitu, uweje muhimu kwangu?


tamathali ya bajeti 2012/2013

Dokta na doktori

 DOKTA ni wa kupewa, doktori kasomea,
Udokta ni hidaya, zawadi watu hupewa,
Hajui au ajua, ukuruba huliliwa,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Barua ukichukua, vyema ukaangalia,
Tarishi bora ukawa, katika yako dunia,
Hili utazawadiwa, dokta nawe ukawa,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Hata anayefagia, pasibakie udhia,
Kila kona ikang'aa. ma vizuri kunukia,
Huyo naye ni sawia, udokta akapewa,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Choo ukiangalia, usafi kutopungua,
Pasiwe nayo kinyaa, pia na harufu mbaya,
Dokta budi ukawa, watu tukakusifia,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Mganga uliyetimia, unajua kuagua,
Wagonjwa kuwatibia, afya ikarejea,
Udokta ukijaliwa, ni halali inakua,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Doktori hutokuwa, hadi kwenda kusomea,
Shahada nayo ukiwa, uzamili 'meingia,
Utafiti ukazua, na majibu kuyatoa,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Unatakiwa kubukua, na nukuu kuzitia,
Kichwa ukakisugua, hadi kipara kutia,
Halafu ukatetea, hicho ulichogundua,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Ubigwa utaridhiwa, kwa mengi sana kujua,
Eneo dogo  likawa, nje-ndani walijua,
Hata unaposinzia, majibu sahihi watoa,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?

Mlevi hautokuwa, ovyo kujiropokea,
Husema wanaojua, majibwa makali huwa,
Kuliko ya muangaliwa, ili kuficha kadhia,
Kumbe iko tofauti, dokta na doktori ?




Ili fisadi kulinda


IPO nia, ipo njia, hawawezi niachia,
Mimi wanitegemea, ya kwao kujilindia,
Nani watamuachia, salama wakabakia ?
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Hamuwezi kuyajua, jinsi nilivyowanyanyua,
Hata watu kuibia, ili nchi kuchukua,
Miezi niliumia, kofia wapate vaa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Yamini tukajilia, awali wewe ingia,
Na wa pili nitakuwa, dhahiri kurudishiwa,
Kila nilichotumia, na ziada kupatiwa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Pembeni tulifagiwa, ili tohara kutia,
Wagomvi wakaambiwa, waache ya kuyazua,
Na timu zikaingia, ili langu ndilo kuwa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Dhahabu waliojaa, yapaswa kuongezewa,
Benki walopakuliwa, sahani kuongezewa,
Miradi waliopewa, yabidi kupanuliwa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Na tuliojijengea, ulinzi unatakiwa,
Ya kwetu tukajilia, bila ya kusumbuliwa,
Na mimi chaugo nawa, hata nyie mkikataa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Mihela sasa yajaa, kila kona twapakua,
Nasibu tumezizua, kila siku zaingia,
Tayari twajiandaa, siku itapoingia,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Sura yangu yasifiwa, waiona maridhia,
Kingine sikuumbiwa, ila rais nikuwa,
Na sasa ninasomea, masta ya ushujaa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Imani nitapindua, na mioyo kuitwaa,
Nisiate kutangia, vikoba vyao kujaa,
Kwa langu mie ikawa, chaguo lisilo waa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Ukubwa ni majaliwa, na udogo naridhia,
Ila ukiangalia, namna ninavyokaa,
Utaona ninapwaya, juu zaidi yafaa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Juu nilipopandia, teke ngazi nikatia,
Wengi wameninyanyua, chini nikawatupia,
Rahisi waliokuwa, ndio niliowafaa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Ya baba nilikataa, nikaona yakuzua,
Ninazidi kushupaaa, ukuu kukuakua,
Ibra kuchaguliwa, si ajabu Tanzania,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Labda akitokeya, madoa asiyekuwa,
Na hilo nitashangaa, kati yetu wajamaa,
Bepari tumeshakua, na madoa ni tabia,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!

Bepari tumeshakua, na madoa ni tabia,
Kama duma na madoa,  hawezi vingine kuwa,
Huyo ukijionea, ni marara atakuwa,
Ukubwa nitaupewa, ili fisadi kuhami!


Cheo nimefinyangwa



Mrithi nimeambiwa, mwingine hawezi kuwa,
Nimefinyangwa radhia, na kiti nimewekewa,
Ni chaguoa la balaa, siku yangu nangojea,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Ni chaguo la nazaa, kwa cheo kukichukua,
Matapishi kuyazoa, chakula kikarejea,
Wala pasiwe kinyaa, watu wawe washangaa,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Ni chaguo la hidaya, na tunu kuzawadiwa,
Na vibwebwe vikatia, karamu kuandaliwa,
Na dini za butwaa, zisiache kuchangia,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Ni chaguo la makaa, majibu yalobakia,
Na masinzi kusingia, machoni wanja yakawa,
Na aibu na vihaya, vijae katika kaya,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Wenye njaa hununua, hata juu walokuwa,
Busara kuwapindua, uzuzu nikawatia,
Na hekima kuing'oa, maghofu yakabakia,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Sina ninayemhofia, ila kalamu ni baa,
Hasa zikijaujua, ukweli ninaojua,
Na nia kuzifukua, kuiuza Tanzania,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Udhalili nakataa, masimango yatazua,
Si wa kupambanua, na pepo kuangalia,
Na yazukapo mapya, siwezi kuyaezua,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Cheo nyumba ya hadaa, ni nani asiyejua ?
Roho njema si shujaa, yatakiwa roho mbaya,
Haya yangu majaliwa, ninaona ninafaa,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Watu ukiwapa raha, mimi huwa naumia,
Nawatakia balaa, tena wazidi umia,
Moyoni kwangu furaha, rahisi kuabudiwa,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Rahisi kuabudiwa, na ukubwa kuutwaa,
Kidogo ukitumia, bwerere kujivunia,
Hadi vyungu vikajaa, na mengine kubakia,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Nna raha ya kuachiwa, moto kutokumbatiwa,
Na vijinga kuving'oa, na vikuni vya kutia,
Wakati ukifikia, nao moto ukapoa,
Cheo nimefinyangwa, ni mimi tu kuachiwa !

Urais nalilia


Jamani mngelijua, nchi mngeniachia,
Nina zangu ruia, zatakiwa kutimia,
Rais nisipokuwa, madeni yataniua,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Sina uchu nawambia, ila nimeandikiwa,
Lakini inatakiwa, nyie kunisadia,
Na shilingi nazitoa, milango kuifungua,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Uroho nimekataa, ili hiwa yangu hawa,
Hamjui ninajua, kutoka na kuingia,
Urais kwangu hewa, bilayo siwezi pumua,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Ulafi sikujaliwa, ila watu kutumia,
Kisha nikawachafua, ya kwangu kufanikiwa,
Na vidonge navitoa, dawa na visivyo dawa,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Watu watanikimbia, rais nisipokuwa,
Muhibu ninahofia, hata naye yumo pia,
Kwangu kizaazaa, siombi likatokea,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Dishi limeepuliwa, mezani linaingia,
Na wa kwanza kupakuwa, ni mimi ninatakiwa,
Wengine kuwazuia, swahibu mnatakiwa,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Magazeti nanunua, redio, tivii pia,
Sura yangu kutumia, ila nisiposinzia,
Magari mtapatiwa, hata juu mkapaa,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Machiavelli radhia, ushauri natumia,
Hulazimika kuua, Macbeth anajua,
Ufalme kuutwa, mizuka kutohofia,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !

Urais ni tabia, haiba na kujongea,
Siwezi kukata nia, labda sijazaliwa,
Gele wanaonionea, nyota hawatatungua,
Urais nalilia, ndoto zangu kutimia !


USINIPENDE MAITI


Nienzi nikiwa hai, ningali ninapumua,
Kuniafu jitimai, na langu kulisikia,
Na dua kunistahi, dhambi nikapunguziwa,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Njoo unigee rai, na afua si mafua,
Sautiyo iwe nai, nikapata kusinzia,
Ni yanini baibai, na nyuma wanifatia ?
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Yako yawe ni anwai, wasipate kusikia,
Niletee na mayai, kienyeji yalokuwa,
Nikaangie na chai, pamoja na kitumbua,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Nipende ukijiwahi, waona nakwangalia,
Na mcho hayatulii, kope  yafuatilia,
Kama unayo madai, usiache kumbushia,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Nipende ninafurahi, moyo ukakuridhia,
Na kama ni asubuhi, karibu ukajongea,
Tupate staftahi, wawili tunaongea,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Naugua, siugui, hali yangu kuijua,
Madhali ningali hai, tunawez kuongea,
Ujualo silijui, laweza likawa dawa,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Naweza nikawa hoi, kukuona nikapoa,
Ana ibra Muhyi, huwezi kuziagua,
Ghaibu hazitulii, ukaribu zakataa,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Nikiwa ni goigoi, waweza kunichapua,
Hilo haliwi jinai, si shida kulitambua,
Moyowe siuchukui, mwilini utabakia,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Mimi sio Mmasai, maiti kuikimbia,
Ila sababu sijui, maiti kuchungulia,
Nifateni niko hai, mfu sintawasikia,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Ila sababu sijui, maiti kuchungulia,
Yangu ninatoa rai, mapema kuifukia,
Islamu na jamii, nakataa kukawia,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Wachamungu nawasihi, ombi langu kusikia,
Msitafute rai, tosha dua kuitia,
Na ubani pia udi, msiache nichomea,
Nipende nikiwa hai, usinipende maiti !

Hayat Bob Makani



Inna lillahi waina illahi rajiuuni,
Bob Makani hatuna, kaondoka muumini,
Twamuombea Rabana, ampe yake hisani,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

kaondoka duniani, baada ya udhamini,
CHADEMA  kuiauni, na kuijenga makini,
Sasa ni chama cha kuwini, kutawala mjengoni,
Rejeo ni kwa Manani, viumbe wa duniani,

Heshima yake kuwini, budi kwenda vijijini,
Huko ndiko mizizini, kwenda ijenga imani,
Wajue yake amini, kuwatoa mashakani,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Tumebaki duniani, kuwafaa masikini,
Pia nao waumini, watokao kila dini,
Wote sisi kwa imani, mmoja twamuamini,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Watu  hawakuwazaini, ili yake waamini,
Awafanzie utani, wakaikosa amani,
Hakuitoa yakini, lililo kuwa shakani,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Ni Gavana wa zamani, kaishi kimaskini,
Ufisadi kauhini, akaijenga imani,
Hakuongeza madeni, nchi kuwa taabani,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Kayaingiza chamani, vijana kuwaamini,
Kawatilia ubani, wawe safi waumini,
Wasiwe kama wahuni, tuwajuao nchini,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Kakaa nao kundini,kuwapa wake undani,
Waende namna gani, watu wakawathamini,
Ikiwa hapa mjini, pia huko vijijini,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Muulize Freeman, mwalimu kamuamini,
Zitto kwenda ughaibuni, ushauri kauthamini,
Tundu kijana makini, anawafunza bungeni,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Na ishara zote nchini, watu wanawamini,
Wengi wao wanadhani, wengine ni watu duni,
Kushika nchi mwakani, hawa ni kuwadhamini,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Ameondoka Makani, kaacha chama makini,
Ikishachorwa ramani, na vijiji kuauni,
CHADEMA wakaamini, ndio yao afueni,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Atafurahi Makani, alofanza duniani,
Tukamlipa hisani, matunda kwa kuyawini,
Demokrasia nchini, isiwe tena shakani,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !

Mtimizie Manani, huyu wako Muumini,
Ya ukweli kaiamini, moja kwa moja peponi,
Na wajue muumini, chama hakina udini,
Hayati Bob Makani, kalale pema peponi !



Iwapo harufu mbaya



MAJENGO wajijengea, bustani zisokuwa,
Chini mashimo yajaa, na kinyesi kunukia,
Uchafuu unazagaa, kote ukiangalia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Uzuri unaovia, waenea Tanzania,
Maji yalikopotea, na mitaro ya balaa,
Usafi ulikofia, na maiti kubakia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Huna utapoingia, kwenye ya umma mitaa,
Akili zikakwambia, hawa watu wamekuwa,
Ni unyama umejaa, kwa siha nayo afya,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Amana waliopewa, sawasawa imekua,
Kipindupindu maua, yaachiwa kuchanua,
Wageni wajionea, na kumbukumbu kutia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Kurudi kwao nazaa, kueuka ya kinyaa,
Kwingine hujiendea, usafi wanakojua,
Ni miji ya majaliwa, kitu isiyojaliwa,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Majengo sasa yang'aa, ila miji yafubaa,
Usafi utaujua, ndani tu unapokuwa,
Nje kote ni balaa, ndio yetu Tanzania,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Harufu inasambaa, hadi ndani kuingia,
Hadhari hatujajua, kukieneza kinyaa,
Imebaki mazoea, na watu wavumilia,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitanuka !

Naimba sikuumbua, ukweli watu kujua,
Hali hii kuachiwa, twaelekea kubaya,
Watalii kukimbia, sifa mbaya kuenea,
Iwapo harufu mbaya, kila kitu kitavia !

Ila ninachokijua, usafi ni manufaa,
Ni huduma maridhawa, uchumi inanyanyua,
Usafi hununuliwa, mapesa yakaingia,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Usafi unavutia, biashara zikakua,
Watu wakikuridhia, nyumbani kwako kukaa,
Wawekezi kuingia, mitaji wakaitoa,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !

Uchafu ukizidia, hata nzi hukimbia,
Maafa yakaingia, ya maradhi na ukiwa,
Kidogo mlichopewa, hata nacho kupotea,
Iwapo harufu mbaya, watu watatukimbia !


Mla vya ovyo hunuka



Hutoacha kumtambua, mla vya ovyo hunuka,
Katu haitatokea, uoza ukamtoka,
Hawezi akanukia, kunuka yake hulka,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Asije kukaribia, roho ikajachafuka,
Sio wanaovutia, karibuwe wakifika,
Ndipo utawachukia, mkono kutowashika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Usafi wawaambaa, mioyo kuwacharuka,
Uchafu waufatia, na uoza wakashika,
Kisha wakatarajia, na watu kukubalika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Wanashindwa jitambua, ni bidhaa wauzika,
Bei ukiigundua, rahisi kununulika,
Si aghali nakwambia, milioni hutofika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Yao yote yanavia, si wa kutamanika,
Za mkato zao njia, chooni zinapofika,
Na harufu huchukua, hadi mbali ikafika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Maji wanayakimbia, na sabuni kutoshika,
Kila wakijichambia, mkononi vinashika,
Kila ukiwachungua, hauwezi malizika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Kalamu naiachia, mbali siwezi kufika,
Tohara naihofia, isije kumalizika,
Najisi ninaiambaa, isije kukanyagika,
Mla vya ovyo hunuka, hilo hawezi kimbia !

Meli tunayosafiri



Wajifanyao jeuri, na kiburi kujitia,
Ninawapasha habari, meli tuliyoingia,
Ni ya kwetu manowari, moja tunayotumia,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Katikati ya bahari, ya hii yetu dunia,
Tukiwamo twasafiri, tunapaswa kutambua,
Iwe heri, iwe shari, bado moja yetu njia,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Yatupasa tafakari, kila tunaloamua,
Yetu kufanza shauri, maamuzi kuyajua,
Vinginevyo ni hatari, hata nahodha ukiwa,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Safari ina hatari, na majanga ya blaa,
Watekaji waabiri, baharini wamejaa,
Nia yao sio nzuri,waweza tuingilia,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Kuchukua tahadhari, yafaa kuzingatia,
Mabaharia hodari, lazima kuajiriwa,
Sio watu wa hiari, kazi wasioijua,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Tukiianzisha shari, wote tutaangamia,
Haramia wakijiri, wote wakatuchambua,
Sote wakatuadhiri, na   vyetu kutuibia,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Kwenye meli kuna chori, inafaa kuwajua,
Na hawa sio kachori, tofauti kuijua,
Hawa ni watu hatari, ni wezi wa kuzaliwa,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Wajifanya wasafiri, usiku wakingojea,
Kisha wakazusha shari, na vitimbi kuvitia,
Watu kutia kabari, au meli kupindua,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !

Ya mapenzi manowari, hii yetu yatakiwa,
Tusifanziane shari, mitegoni kuingia,
Ikatukimbia heri, mashakani kuingia,
Meli tunayosafiri, moja, MV Tanzania !


Kadhi amehudhuria




kadhi amehudhuria, mazishi ya Saitoti,
Na katoliki kakaa, Kenya na wao hayati,
Hapa kwetu Tanzania, waumini wasaliti ?
Mazishi ya Saitoti, Kadhi amehudhuria !

    Imani imezuliwa, na uongo katikati,
    Wakuu wakasikia, yake leo hayapiti,
    Sasa ni wadhulumiwa, na wakati hausiti,
    Mazishi ya Saitoti, Kadhi amehudhuria !

Waumini ninajua, idadi hawaikuti,
Ni kidogo walokuwa, Kenya haina umati,
Ila haki wamepewa, kadhai amepewa kiti,
Mazishi ya Saitoti, Kadhi amehudhuria !

    Na dua ameombewa, ya watu wa misikiti,
    Udugu wazingatia, hakunayo hatihati,
    Ila sisi Tanzania, kwa fitna hatupatwi,
    Mazishi ya Saitoti, Kadhi amehudhuria !

Nadra mafanikio


UONGO palipojaa, vigumu kufanikiwa,
Ni jangwa palipokuwa, kitu hakiwezi mea,
Hupakimbia mvuu, ukame ukazidia,
Vigumu kufanikiwa, palipojaa uongo !

Fisadi walipojaa, kuifasidi dunia,
Kila kiumbe hunywea, na mioyo ikavia,
Huruma ikapotea, pakabaki maasiya,
Mafanikio nadra, palipojaa fisadi !

Watu wakiwa bidhaa, rahisi kununuliwa,
Malaika hukimbia. pembeni kujikalia,
Mungu wakamlilia, haki yake kuitoa,
Vigumu kufanikiwa, watu wakinunuliwa !

Zikiingia sanaa, maisha kuyatania,
Uhai mara huvia, na mioyo kudumaa,
Pasiwe la kusikiwa, sembuse kufanikiwa ?
Mafanikio nadra, palipo na usanii !

Uonevu ukijaa, chozi dunia hutoa,
Ardhi 'kajinamia, watu kusikitikia,
Na mbingu kujipasua, kwa hasira kuijaa,
Vigumu kufanikiwa, uonevu ukijaa !

Dhuluma ikiingia, nchi huwa yatitia,
Na bahari kutanua, nchi ikaivamia,
Kilio kikasambaa, hata ng'ambo kufikia,
Vigumu kufanikiwa, dhuluma ikitawala !

Watu wanakozomea, bila kitu kuelewa,
Vitabu  hujifunua, orodha ikaitia,
Wajinga waliojaa, hadi nchi kulemaa,
Vigumu kufanikiwa, watu wanakozomea !

Roho zikiwa bandia, unafiki ukajaa,
Mazuri huwakimbia, yakabakia mabaya,
na uoza ukajaa, kushoto pia kulia,
Mafanikio nadra, kwa mapambo ya bandia !

Rushwa ikivumuliwa, kama halali ikawa,
Askari na raia, hofu ikawapotea,
Kwao kuwa manufaa, riziki kujipatia,
Vigumu kufanikiwa, rushwa ikivumiliwa !

Ubaguzi ukiingia, vyovyote unavyokuwa,
Kwa koo kuzingatia, au siasa zikawa,
Rehema hujisanzua, mbali na watu kukaa,
Mafanikio nadra, palipo na ubaguzi?

Upendeleo balaa, wa ndugu nao jamaa,
Kila unapoingia, hauachi kuchafua,
Vitu vyote kusinzia, hadi rivasi ikawa,
Vigumu kufanikiwa, palipo upendeleo !

Umbeya palipojaa, wema watapakimbia,
Ikabakia nazaa, mafuu pia vichaa,
Bure waliozoewa, riziki kujipatia,
Mafanikio nadra, umbeya palipojaa !

Kashfa zinapojaa, huota mkubwa waa,
Madoa yalotitia, kazi kweli kuyatoa,
Fisadi gamba kuvaa, uchafu ndani ukawa,
Vigumu kufanikiwa, kashfa zikifukiwa !

Haki ikununuliwa, sheria inalemaa,
Imani ikapotea, majaji kudharauliwa,
Na vyombo vikakimbiwa, watu peke kubakia,
Mafanikio nadra, haki ikinunuliwa !

Masikini wakiibiwa, husikitika dunia,
Na machozi ikatoa, haki kuwapigania,
Si kazi kujipindua, miguu juu ikawa,
Vigumu kufanikiwa, vya fakiri vikiliwa !


Tabia hii si njema


Haifai maamuma, na pia ina imamu,
Dhambi bure ukachuma, kwa yasiyo umuhimu,
Katika zenu kalima,na vitendo kuvikimu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Wapo wasiyo rahima, watu wanaodhulumu,
Kwa kujifanza adhama, na eti watu muhimu,
Dunia wakaihama, hali sio marhumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Ya dini wakayakama, na kuyatia hukumu,
Akili zikawahama, zikatinga jehanamu,
Ya uongo kulalama, ya wengine yawe magumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Kioo hujitazama,  wengine kuwahukumu,
Yawaishia hekima, imani kuzihasimu,
Na Mola ni muadhamaawajua  mahadhamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Huichezea neeema, kufanza wengi hadimu,
Wakajitia karama, zimekwishawasalimu,
Na yao bila kusoma, yaweza kutakadamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Hawaipata karamu, na wengine hudhulumu,
Akaitoa Karima, kwake walio rahimu,
Wakaifanza hujuma, kuhukumu binadamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Ukubwa huuazamia, wakajifanza kaimu,
Nchi wakaisakama, ya kwao yapate dumu,
Wakazizua nakama, tena daima dawamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Hakika hawajasoma, ya kheri wayashutumu,
Busara zinshawahama, na ualimu adimu,
Upofuni wanazama, nia yako kukirimu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Dunia itasimama, kwa wao kuihumu ?
Yake yeye wamehama, na sanaa waadhimu,
Kinawangoja kiama, kikawafanza karamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Haitozama neema, kwa layli na kiamu,
Zitafutika hujuma, fitna za wanadamu,
Kwao ikawa gharama, na wenyewe madhulumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Mioyo itaegema, kumtwii ya Karimu,
Na palipo na zahama, akaondoa ugumu,
Kwetu yakawa uzima, na kwao ni marhumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Yatakuja kusimama, wao wasiyo azimu,
Muumini akasoma, na kuzijua hukumu,
Ikijaiika rehema, heri wakaisalimu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Waipatao heshima, wengine hawahukumu,
Na walio na hikma, wengine hawadhulumu,
Na mtu kuwa salama, ya watu asihujumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Utukufu wa Alima, mkuu wa mahakimu,
Yake ndio husimama, sio wanaodhulumu,
Kiumbe aso rehma, yake huwa hayadumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Waipatao heshima, wengine hawahukumu,
Na walio na hikma, wengine hawadhulumu,
Na mtu kuwa salama,ya watu asihujumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Hizi ni nyingine zama, kafiri wanasilimu,
Mtu hapati heshima, kwa majoho na kalamu,
Kama anayoyasema,yanukia udhalimu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Waipatao heshima, wengine hawahukumu
Na walio na hikma, wengine hawadhulumu,
Na mtu kuwa salama,ya watu asihujumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Au wanaojinoma, na kujifanza rahimu,
Hadaa wakazitema, na umbeye kukirimu,
Huzaa yao lawama, yalojaa Jahanamu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Waipatao heshima, wengine hawahukumu,
Na walio na hikma, wengine hawadhulumu,
Na mtu kuwa salama,ya watu asihujumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Hapa ninatia tama, muda nisiwadhulumu,
Tuitafute rahma, kwa umoja kuukimu,
Wamoja tukisimama, yatakwisha madhulumu,
Tabia hii si njema, ya riha na kujiona.

Thursday, June 14, 2012

M W A N A M K E U S I M W I T E



Mwanamke mwite pusi, wito atausikia,
Atayafanza mepesi, magumu ulodhania,
Akatia udamisi, utakalo kujaliwa,
Mwanamke umwiite, pusi wala sio paka !

Ukimwita yeye paka, aweza kukurarua,
Makucha akakutia, viungo kukunyofoa,
Na meno akakutia, na nyama akaitoa,
Mwanamke umwiite, pusi wala sio paka !

Mwite mwanamke njiwa, hana budi kukujia,
Na begani akatua, la kwako kulisikia,
Huku tena asinzia, na macho kuyarembua,
Mwanamke umwiite, njiwa wala sio kuku !

Thubutu umwite kuku, kama hatokurukia,
Huruka huko na huku, akawa akudonoa,
Huwezi mfunga luku, mita zake hukimbia,
Mwanamke umwiite, njiwa wala sio kuku !

Mwanamke mwite toto, witowe atasikia,
Huenda ikawa ndoto, yake kwako ni ruia,
Na baridi kuwa joto, kwa ndani umetulia,
Mwanamke umwiite, toto ila si mtoto !

Ole, umwite mtoto, mawe  atakutupia,
Ukapata mkong'oto, na nundu kuzawadiwa,
Iwe ni yako majuto, neno kutokurudia,
Mwanamke umwiite, toto ila si mtoto !

Mwanamke mwite bonge, wala hatokuringia,
Huzubaa kama tonge, kinywani likichelewa,
Na shuleni mwenye nunge, uhodari kujaliwa,
Mwanamke umwiite, bonge wala si mnene !

Usimwiite mnene, hilo hatofurahia,
Mengine usiyanene, moyoni ataumia,
Nzige sio senene, kufanana haijawa,
Mwanamke umwiite, bonge wala si mnene !

Mwanamke mwite miss, kama mwembamba akiwa,
Huyo katu hakususi, cheo umempatia,
Atakuminya chunusi, na ndevu kuzichezea,
Mwanamke umwiite, 'kimisi' sio ukuni !

Ila njiti 'kimwambia, mbali nawe atakaa,
Moyoni kuugulia, Uzungu usikokuwa,
Biashara ikavia, mswahili kususia,
Mwanamke umwiite, 'kimisi' sio ukuni !

Mwanamke ni kijinga, mwana anayeutoa,
Kwa hayo ukimlenga, katu hatokuachia,
Wala tena hatoringa, yako unapomwitia,
Mwanamke umwiite, kijinga wala si mwanga !

Usije mwiita mwanga, daima hukuchukia,
Japo kajaliwa wanga, na azidi kuchakaa,
Yeye nuru sio mwanga, hawezi kukuelewa,
Mwanamke umwiite, nuru lakini si giza !

Mwanamke ni Chepe, hata Fataki ajua,
Hatolikosa la lepe, usingizi kumjia,
Roho ikawa nyeupe, kwa wito kuuridhia,
Mwanamke umwiite, cheupe wala si kupe !

Ukimwita yeye kupe, yako atakususia,
Hata vipi uongope, tena hautomrudia,
Hulipiga lake chepe, nasibu kuifukua,
Mwanamke umwiite, cheupe wala si kupe !

Ukimwiita bleki, uzuri hujisikia,
Masikini mamluki, lugha njema kudhania,
Akawa nayo ashiki, ya kwako kuyasikia,
Mwanamke umwiite, blaki sio mweusi !

Ni heri umwite cheuisi, kuliko awe mweusi,
Ataona ni nuksi, kiumbe kutojijua,
Akapunguza maksi, kwa kuutia  mkasi,
Mwanamke umwiite, blaki sio mweusi !

Mwanamke bwana jina, moyo utauchukua,
Ikawa yako amana, ndani umeichukua,
Pasiwe kwenye hiana, maisha kufurahia,
Mwanamke umwiite, jina wala si majina !


Mama kakwambia kweli ?

AKILI wasiopewa, ujanja huutumia,
Yake kuwa, huwagawa, tena pasi kujijua,
Akawa achekelea, wajinga mlivyokuwa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Ndio nakuulizia, kama hili unajua,
Wengi huwa wabomoa, sana watu kama hawa,
Tena mkubwa udhia, nyumbani wanapokuwa,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Huru ukiwaachia, hawana demokrasia,
Udikteta huzua, waliko kujivutia,
Kuachia hukataa, hata wakikataliwa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Huzua wanayozua, na uongo kuutia,
Na aibu wala haya, kamwe hawakujaliwa,
Moto wanauhofia, lakini wasogelea,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wazuri wa kutumia, hata mnapoishiwa,
Nderemo yao nazaa, na kesho yao mafua,
Mazuri huyakimbia, wakavamia mabaya,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Kawaida humtokea, ila sio mazoea,
Na mitume nao pia, haya wanasimulia,
Mwema unapozaliwa, zawadi yako mbaya,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Ni nani kakuambia, baba aweza kujua,
Hii ni ngumu sheria, yashinda wanasheria,
Si Mchagga ungeria, ndio kwanza ukatoa,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Masikio watakiwa, vyema ukayatumia,
Kila unalosikia, usiache kuchungua,
Ukweli unafukiwa, watakiwa kufukua,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wapo walio vichaa, tayari wamewazaa,
Nje hutomdhania, ila kwa ndani yakawa,
Kiatu kinachopwaya, guu kinaliachia,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Twavaa zetu kofia, uongo zilizojaa,
Humjui, akujua, ndivyo ilivyo dunia,
Hushikwa wasiokuwa, na walo wakaachiwa,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?

Wapo wanayoyavaa, mawani yao ya jua,
Na rangi iliyokuwa, nakshi ikaitia,
Nyeusi iliyokua, na vitu kuwapotea,
Mama kakwambia kweli, au huna ujualo ?

Kama kasha ingekuwa, mioyo tukafungua,
Mengi tungejionea, ambayo hatujaambiwa,
Na hii ndiyo dunia, mengi hatutayajua,
Mama kakwambia kweli, au kesha kupotosha ?


Kanga ovyo nimekaa



Kanga nimekasirika, kitenge kanichengua,
Bila aibu kamaka, uzuri kanizidia,
Na bei juu kaweka, siwezi kumfikia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Akazidi kubwetuka, hata ndani aingia,
Pazuri wakamuheka, bila kusumbuliwa,
Kabatini akafika, au sandukuni kukaa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Ila mimi sina mwaka, kila pembe natupiwa,
Ndani yanayofanyika, aibu najionea,
Heshima imetoweka, ninavydharauliwa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Mafichoni huniweka, mwenzenu nikaugua,
Nikataka kutapika, na mbali nikakimbia,
Ila wanavyonishika, ni viumu kujiondoa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Kidogo nikichanika, kazi nyingine napewa,
Kitenge atatibika, na kiraka kuwekewa,
Mie ninafadhaika, humo ninamoingia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Siwezi kusetirika, ni aibu nakwambia,
Na kitenge aropoka, umbeya alivyojaa,
Hivi sasa nasifika, mhifadhi wa shubaka ?
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Natamani kuokoka, vingine kuvikimbia,
Namtafuta Mayoka, na Liganga kuwambia,
Na nyumbani kutambika, kuliepuka balaa,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Mwenzenu naghadhabika, karibu kuwa kichaa,
Hakika ninaudhika, wapendavyo kunivaa,
Na waganga wanishika, na uchafu waniachia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Wachawi wananitaka, kwa yao kunitumia,
Mzima wananizika, na chini kunifukia,
Watoto wasiotaka, yao wanipangusia,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Kitanzi nikikitaka, kibao wageuzia,
Wao wende kujizika, na mimi nikabakia,
Ninaitwa wa kuchoka, watu wanajinyongea,
Kanga ovyo nimekaa, kitenge kahifadhiwa !

Usiende na kababu



NAMI nieje bajia, ni nini cha kunisibu,
Kababu wamchukua, unaniacha naibu,
Na sote tumebukua, hadi huko Ughaibu,
Usiende na kababu, nami nieje bajia ?

Ni chache zangu wakia, ila ni kitu  muhibu,
Wahindi hunililia, kwa kukosa uraibu,
Pilipili nikitiwa, wala siwi na ghadhabu,
Usiende na kababu, nami nieje bajia ?

Mkate kashindiliwa, hana aibu kibabu,
Na nyama kahujumiwa, mla mboga hana jibu,
Na unga hajaujua, keshamuhini Mwajabu,
Usiende na kababu, nami nieje bajia ?

Kababu kahifadhiwa, sura yake ya  ajabu,
Kwa moja hakutulia, sembuse kutaadibu,
Sura zote huchukua, nyingine bila hesabu,
Usiende na kababu, nami nieje bajia ?

Bajia namshangaa, hana majibu ya ghibu,
Kila kitu akamia, na kumla nako taabu,
Pilipili akitiwa, utadhani mraibu,
Usiende na kababu, nami nieje bajia ?

Jimbo hili nimepewa



Mimi piwa mswahili,  Manani kanijalia,
Ni lugha yangu asili, toka nilipozaliwa,
Hata sasa nahimili, umma kuuandikia,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukilinda !

Ninaiona kamili, utajiri imejaa,
Hii lugha ya halali, haramu yaukataa,
Kwangu ni kama kandili, njia yaniangazia,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukienzi !

Inaweza ya awali, na ya akheri yakawa,
Rijali na wanawali, kwa yote kuwaandaa,
Wakifika ngazi ya pili, lugha ngeni wakajua,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukijenga !

Watoto wana akili, lugha haitochentua,
Waweza wasome mbili, hata na ya tatu pia,
Ya msingi mahafali, ikwa tatu wajua,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukijenga !

Na hiyo ngazi ya pili, kazini wanapokuwa,
Ili kufata ya mbali, wapaswayo kuyajua,
Waende kuyanakili, kwa Kiswahili yakawa,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukilinda !

Wachina hili wajali, yote sasa wanajua,
Hao ni watu kamili, si nusu waliokuwa,
Sisi bado ni kivuli, utu hatujatambua,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukienzi !

Amkeni bilkuli, majimboni mlojaa,
Bongo zijibu maswali, lugha ipi kutumia,
Hali wa kwenda mbali, Kichina budi kujua,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukijenga !

Kiarabu afadhali, herufi tukipindua,
Mwandiko wa Kiswahili, hazina itafukua,
Ama sabini na mbili, yatimu asilimia,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukilinda !

Maneno ya Kiswahili, Kiarabu yalokuwa,
Ukifanza udahili, kamusii mbili watoa,
Jamani hii si mali, yatosha kujifunzia ?
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukienzi !

Nilishasema awali, hadimu hatojaliwa,
Ili kulikabili, na kweli likatokea,
Alaa, hii ndiyo hali, nchini najionea,
Jimbo hili nimepewa, Kiswahili kukijenga !


Banda langu la udongo



LA udongo banda langu,  ukibomoa najenga,
Haiishi siku yangu, upya nitalipanga,
Wala sio hofu yangu, tetemeko likigonga,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Ni tulivu moya wangu, utadhani ninaringa,
Supa ufakiri wangu, kwa mtu sijajigonga,
Na waridhi ua langu, weupe  lililoviringa,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Yapeta mapenzi yangu, yafanzika kwenye changa,
Wasiwe saizi yangu, kwenye ghorofa kutinga,
Maisha ni raha yangu, ukiwa haujanizonga,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Dagaa chakula changu, lishe yake kama manga,
Mchuzi wangu wa dengu, na wali ninauchonga,
Kahawa yangu ya kungu, mato yangu kuyakinga,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Ni tamu hisia zangu, hakuna anayepinga,
Wajua utamu wangu, hautoki kwa mganga,
Hawa ni asili yangu, kurogwa nimejikinga,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Haya ni maisha yangu, wataka nini kulonga,
Haujui moya wangu, na lipi nililopanga,
Hiyo ndugu siri yangu, kwako katu ha'totinga,
Banda langu la udongo, nilihofu tetemeko ?

Lipi wakusaidia ?



Wasiwasi waugua, kitako kutotulia,
Mwanangu nakwambia, ni bure yako fadhaa,
Huna unalougua, ila kisaikolojia,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Hayo ukiyakataa, uzima ukajitia,
Hutoipata fadhaa, na moyo utatulia,
Ila ukiendelea, pabaya utaingia,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Moyo fanza kuridhia, la Mola huja timia,
Hofu unapoitia, bure unajionea,
La kuwa budi likawa, lisokuwa, kutokuwa,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Bure unajisumbua, la kuwa budi likawa,
Hapana wa kuzuia, lazima litatimia,
Kadari ukiijua, Mola utamuachia,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Madogo kutokukuzua, makubwa ukaachia,
Jengo ulilojaliwa, wapaswa kuangalia,
Ni mwili uliopewa,  na Mola wetu Jalia,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Udokta aujua, hata hewa kuwa dawa,
Na dua ukizijua, balaa huliondoa,
Huko ukishazamia, hofu utaiondoa,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Umri nakuombea, nyuma ukanifatia,
Mazuri kuja kuzua, nchi ikajivunia,
Nawe budi kutulia, Mola ukamuachia,
Lipi wakusadia, wasiwasi wako bure !

Dhihaka n'ache kutoa



Nimekwishajichumia, kivulini ninakaa,
Na kila siku natia, vyote vinavyokolea,
Nani wa kumfikiria, bure nikajisumbua ?
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Mtaji nishajipatia, kwa mbovu Tanzania,
Na njia ninazijua, vitu nikajivutia,
Kwangu vikajipitia, kunawiri kwendelea,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Tumbo langu linajaa, masikio yafuaa,
Siwezi kuwasikia, kilio mnacholia,
Sasa najitafunia, niwezeje kuongea ?
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Malipo narudishiwa, mikopo niliyotoa,
Na bure nilivyogawa, wala waliojaliwa,
Nami hivyo changu pia, niacheni kujilia,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Huwezi ukawa dawa, kwa wote kwenye dunia,
Kundi limeshatimia, wengine nawaachia,
Ila nikishaambiwa, budi nitawaumbua,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Dhihaka nitaitia, na mimi nikasifiwa,
Kusema sana najua, maana yasiyokuwa,
Ila kambi kutetea, wa taifa nilokuwa,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Hata mkinichukia, nilikwishaandikiwa,
Yote yangu yatimia, katika hii dunia,
Hayo yakuyangojea, nyie ninawaachia,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Urithi sijangojea, changu nimeishachukua,
Changu wasije kitwaa, ndo hivyo nawatetea,
Nchi inaendelea, ila vipofu mmekuwa,
Dhihaka n'ache  kutoa, tumbo langu linajaa ?

Chama sasa ni mradi


USANII waingia, vyama vinanunuliwa,
Dau kubwa wanatoa, fisadi kuviingia,
Na nafasi kuzitwaa, ukubwa wakajaliwa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Bahasha mnazopewa, ruzuku yenu yaliwa,
Mapya wanafukua, ya zamani kufukia,
Na wajinga wanaliwa, bilal ya kujitambua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Mafuta mnayotoa, wenyewe mwakaangiwa,
Hii ndiyo Tanzania, na majuha ndio hawa,
Kila ukifikiria, hautaiona ndia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Miradi wafikiria, hewani ikaishia,
Hadithi imebakia, vichanga wanavyoua,
Wakabaki tegemea, haamu vilivyokuwa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Biashara twasomea, wenzetu watukataa,
Kujua wanajitia, na haweshi kufulia,
Hadimu wamezoea, ridhaa wanaotoa,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Hawataki walokua, wanakikinga kifua,
Na yao  wakakataa, kufuja yanapokuwa,
Miradi kutojifia, ikazidi kuchanua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Wanataka wenye njaa, kila kitu kwitikia,
Hata na yasiyofaa, wakaja kuyajutia,
Hilo nami nakataa, siwezi kuwasaidia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Kofia ningelipewa, mbona ningewanyanyua,
Kwani mimi si adawa, chama sijakikimbia,
Ila mwafanya nazaa, mtakayokujajutia,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Siasa ni majaliwa, kwa wengine ni vipawa,
Na wapo wasiokuwa, ila mengine wajua,
Akili wanaokua, hili wapaswa kujua,
Chama sasa ni mradi, tena wa watu wachache !

Wabunge wa Tanzania


Shindano: Mchuano wa Kuzunngumza Kiingereza !


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Kiswahili maridhia,  sisi tuliyejaliwa,
Leo kikawa kinyaa,  hakifai kutumiwa,
Shindano naliandaa, Kingereza kuongea !

Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Kuongea mtatakiwa, mada mnapozitoa,
Ung'eng'e tu kutumia, kuanza na kuishia,
Bila maneno kutia, Kingereza yasokuwa !


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Kama ni li moja saa, au yakawa masaa,
Kiswahili kubabia, katu halitokubaliwa,
Ushindi hamtopewa, ila kulipa fidia !


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Sasa nachangamkia, wafadhili kwa mamia,
Lugha wanaoililia, izidi kuendelea,
Ili wapate changia, fuko langu la  hidaya!


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Kiasi nikikijua, fomu nitawatumia,
Mjaze kwa njema nia, shindanoni kuingia,
Kila fomu naambiwa, milioni itakuwa !


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Zawadi zawangojea, majuu kwenda paa,
Mkamwone Malkia, na Buckingham kuingia,
Na siri mkagundua, huko miktembelea !


Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Na siri mkagundua, huko miktembelea,
Kuandika wasojua, Kiingereza waongea,
Kusoma wasiojua, Uingereza wamejaa!

Wabunge wa Tanzania, lugha mnayoiua:
Kasumba ikiwaishia, la kwenu mtalijua,
Aali kuazimia, nchi ipate endelea,
Mzaha nazo nazaa, ktu hazitosaidia !