Monday, December 26, 2011

Kiswahili kitakufa

Hapana wa kukilea, Kiswahili chatitia,
Kimekwisha kulemaa, tena kinachechemea,
Miaka imebakia, michache ilokua,
Kiswahili kitakufa, kwa kuwakosa walezi!

Ni lazima kujifia, kama mende kubakia,
Heshima imepungua, hususan kwa wazawa,
Ya nje wajititimua, ya ndani wanaachia,
Kiswahili kitakufa, na Kiingereza kuoza!

Ujenzi sasa sanaa, na viongozi kusifiwa,
Hakuna wa kunyanyua, tofali la kujengea,
Lugha iliyojaliwa, sasa imelaaniwa,
Kiswahili kitakufa, ya Kilatini kumbuka!

Uchumi unapungua, udhaifu waingia,
Kigiriki chatitia, kina hali hii mbaya,
Nacho kihispania, na kireno nakwambia,
Kiswahili kitakufa, Sanskriti kumbuka!

Kichina juu chaingia, watu wakipigania,
Uchumi wakiinua, na sifa kujipatia,
Watu wataka somea, kesho iwe yao dunia,
Kiswahili kitakufa, Kisyria nakumbuka!

Amkeni Watanzania, dhahabu mshaibiwa,
Na lugha hii nayo pia, dhahabu kuitambua,
Mwaweza kuiumia, ufakiri kupungua,
Kiswahili kitakufa, kwa kukosa fundishia!

Milioni huingia, lugha mkiitumia,
Shule kufundishia, na vitabu kuchapia,
Na penginepo dunia, watakapoitumia,
Kiswahili kitakufa, viongozi mdebwedo!

Mwaendelea zubaa, Wakenya wajichumia,
Zanzibar nayo pia, Kamusi inazizindua,
Nani mnamngojea, lugha kuja inyanyua?
Kiswahili kitakufa, nchi inayosinzia!

Wenyewe mkiamua, kuanza kuitumia,
Vita vitakujazagaa, na kheri vilivyokua,
Mkaja kushangaa, mtakavyofanikiwa,
Kiswahili kitakufa, kuwekeza kwapungua!

No comments: