Rais wa wasiwasi, na lwake asiyejua,
Namuona kinamasi, sio wa kutegemewa,
Kumvaa ibilisi, si vigumu itakuwa,
Asiye lake Rais, ni kiongozi kofia.
Asiyejua kiasi, na lipi la kuchagua,
Humuandama nuksi, hata za wengine pia,
Vigumu kutanafusi, wahaka unavyomjaa,
Asiye lake Rais, ni kiongozi kofia.
Hana bora majilisi, maamuzi kuamua,
Hutanguliza nafusi, akili nyuma ikawa,
Mfalme bila libasi, 'kavaa' akaambiwa,
Asiye lake Rais, ni kiongozi kofia.
Kumbe uchi hajihisi, adhania amevaa,
Na watoto wa nemsi, wakisema hushangaa,
Akatafuta kipisi, stara kujitakia,
Asiye lake Rais, ni kiongozi kofia.
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment