Wednesday, December 14, 2011

Utajiri wa madini

KIngine ingelikua, ningeshayaingilia,
Kwa kina ningepekua, na undani kuingia,
Kisomo ningechukua, nisije kuhadhithiwa,
Utajiri wa madini, ngoja nifikiri kwanza!!!

Nahofia kuuvaa, utajiri wa chimbua,
Sijui nitakamtoa, ni jini au balaa,
Masharti yaniwia, magumu kuyaelewa,
Utajiri wa madini, ngoja nifikiri kwanza!!!

Ghanima nahitajia, ila sijui ipi njia,
Safari ningeamua, wapi nije kuanzia,
Na vijia vya kupitia, hadi fikio kutua,
Utajiri wa madini, ngoja nifikiri kwanza!!!

Naogopa kupagawa, au kuja nizuzua,
Nishindwe kujielewa, na njia kupotea,
Mwenyewe kujiumbua, aibu zikanivaa,
Utajiri wa madini, ngoja nifikiri kwanza!!!

Nachelea kuambiwa, haramu nimechukua,
Na moto nauhofia, kujipalia na makaa,
Wahyi naungojea, la kufanya sijajua,
Utajiri wa madini, ngoja nifikiri kwanza!!!

No comments: