Monday, December 26, 2011

Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

VIPI mtu anakua, kiongozi wa kufaa,
Bila kuchaguliwa, na mila kuzielewa,
Vyeo bure wanapewa, mikoa yadidimia,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Mikoa yadhamiria, mbali kulifagilia,
Tunataka kuchagua, kiongozi wa mkoa,
Waziri mkuu kua, baraza akateua,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Siasa zinatuua, twabeba visivyofaa,
Vyeo sasa tunagawa, pipi sasa imekua,
Wanaokutetemekea, ndio unawachagua,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Wajuao kuzomea, ndio wanaotambuliwa,
Wawezao shangilia, ujinga hata ukiwa,
Na vigelegele pia, kweli watatuongoa?
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Mzigo tunanyanyua, usiotusaidia,
Uchafu wa kufagia, hazina tunautia,
Haya ninashangaa, hata mkinichukia,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Uongozi si sanaa, ni ujuzi watakiwa,
Na mkuu wake mkoa, lazima kuchaguliwa,
Gavana ndiye akawa, waziri mkuu mkoa,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Tunawajaza mamia, ofisi zetu mkoa,
Kazi hawakupangiwa, hakuna wanachojua,
Wakanyagana kwa kuwa, hawana cha kuamua,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Vyeo pacha vimekua, mafuu tumeshakua,
Hakuna linaloendelea, fedha ila zinaliwa,
Mbele hatutasogea, hili likiachiliwa,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

Wakati wa kuamua, sasa imeshafikia,
Waziri Mkuu kua, si mkuu wa mkoa,
Baraza kusimamia, kma nchi kua mkoa,
Sasa waziri mkuu, si mkuu wa mkoa!

No comments: