Friday, December 23, 2011

Nasaba wameikata

Kama vile hana mama, na ndugu nao hakuwa,
Nasaba wamenyima, cheo si chake kapewa,
Na wenye hii kalima, kosa lao walijua,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Hawa ni watu wazima, utoto waliachia,
Nani aliyewatuma, na kwa vipi wanajua,
Mimi lanipa zahama, kweli nawahurumia,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Wapo wanayoyasema, wengine wanatubia,
Wakitata nao umma, kisha wanajifungia,
Na kuikana kalima, wakubwa wamewaambia,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Afrika wake umma, mimi ninawaombea,
Waikatae hujuma, na ukweli kuzingatia,
Ili wapate rehema, uje kutunyanyua,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Shinikizo la nakama, wenzetu watufanyia,
Kwanza ni baba na mama, na sasa ushoga unaingia,
Tuepushe na hatima, ya kuja kulaaniwa,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Shetani amewatuma, wala hawajajijua,
Hili halina ghanima, nyongo lawatumbukia,
Na moto wataukoma, utakavyowashambulia,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Nakuomba ya Karima, macho kujawafungua,
Wakaijua hasama, wanayojiandalia,
Wakose pa kuegema, siku ya kuhesabiwa,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Ah, kunradhi ya Hakima, nashindwa kulingania,
Si watu wenye hekima, ila wewe ukiamua,
Wakichezea kiyama, wanapo kukutaniya,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Kakaze wamewazima, hakuna anayejua,
Ni nguo ya kuazima, mwenyewe kaichukua,
Wanatisha maulama, kwa wanayoyaamua,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Baba wa kambo katemwa, hawataki msikia,
Aliyoyafanya mema, yamekwishakufukiwa,
Wanazidisha huruma, twazidi kuwaonea,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!

Dada zake kawahama, utukufu kuchukua,
Sijui yake alima, au wamepakazia,
Ila sioni neema, nasaba kuikataa,
Nasaba wameikata, mengi kumsingiziya!



© 2011 Sammy Makilla

No comments: