Ninabakwa, nauawa, kisa ni yetu hidaya.
Dhahabu tulojaliwa, wazungu waichukua,
Serikali yawafaa, na mimi yanikataa,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Kilio hamjasikia, bungeni mnasinzia?
Jirani mliokua, mbona mwakaa kimya,
Au mmpewa ubia, kichumo mwajichumia?
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Mbona ninadhulumiwa, hamji kunitetea,
Umekufa ujamaa, na huruma nayo pia,
Babu ninamuwazia, angekuja niokoa,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Kuzimu akisikia, mizuka atashtua,
Kijijini kuingia, kuja kunipigania,
Kwa maumbo yalokua, miye nisiyoyajua,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Bahati naingojea, wakuja kunitetea,
Changu kutodhulumiwa, mikononi kukitia,
Utu nikaukomboa, na heshima yangu pia,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Afueni nangojea, siku ikijawadia,
Kweli nitashangilia, dunia wakanisikia,
Wote wapate kujua, sasa nimerehemewa,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Aibu kuikimbia, na fedheha ilokua,
Sura nikafichua, za hao wapita njia,
Umati kuwazomea, na mate kuwatemea,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Ni heri wakapotea, vyetu wakatuachia,
Wengine watatujia, hila nao wasokua,
Ya kwao yakatufaa, pengine kutunyanyua,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Ni wajinga walokua, bilioni kutumia,
Viumbe kuwanunua, wangapi watatimia,
Wengine watazaliwa, na wito kuendelea,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Mabaaya nawaombea, hali wasiotujua,
Maiti waliokua, ijapo wanatembea,
Shimoni kudidimia, pasiwe wa kuokoa,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Madhambi ninatubia, kutakaswa na radhia,
Dua kunikubalia, akisha kuisikia,
Kwetu ninawambia, kupendwe kwa kuanzia,
Nauawa, ninabakwa, kisa ni dhahabu yetu.
Wednesday, December 14, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment