Monday, December 26, 2011

Kiungo chako kibovu

Kiungo hakina kazi, kuwa navyo ni mzozo,
Watakiwa uamuzi, kupunguza shinikizo,
Apatikane mchuuzi, akufanyie mauzo,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke??

Usiifanye ajizi, zitakwisha pumzizo,
Ubakie ni wajuzi, kwenye haya mazungumzo,
Hali ilikuwa wazi, siku ulikuwa nazo,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke??

Halihitaji ujuzi, liwazi tokea mwanzo,
Ukifanya ubazazi, hufanywa ya mawe nguzo,
Ukabaki simulizi, au pengine tangazo,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke?

Yatakiwa mageuzi, na sio mazungumzo,
Maneno ni upuuzi, zama hizi za chetezo,
Moshi haunao kazi, yatakiwa ya mkazo,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke?

Alama zashehenezi, au kwako maigizo,
Hii ngoma ya maswezi, eti kwako ni mchezo?
Isiwe hatuyawezi, pakatokea uozo,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke?

Mengi yataka kimbizo, mwenzetu wazidi pozi,
Hulijui shinikizo, halinalo kizuizi?
Usituseme kikwazo, kumbe wewe kizuizi,
Kiungo chako kibovu, wang'ang'ana kisitoke?

No comments: