Friday, December 16, 2011

Wanyonyaji na vijiji

Mkulima Tanzania, mengi ameyapitia,
Mkoloni kuingia, kumnyonya kaanzia,
Uhuru kujipatia, kidogo ukapungua,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Mwarabu kawavamia, visiwani akakaa,
Wanyamwezi kuuawa, na wengine kutumiwa,
Mashamba wakaandaa, karafuu ikakua,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Muungano kuzaliwa, Pemba wakazodolewa,
Mashamba waliyopewa, kuchuma wakatumiwa,
Zao lao halikuwa, serikali ikatwaa,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Karafuu ni maua, si bure yajiotea,
Na ya kwao lewalewa, bado inaendelea,
Mwana kazi kumlea, hawezi kukuangalia?
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Kuanzishwa ujamaa, zaidi ukazidia,
Mgongoni kapandiwa, wengine kuwachukua,
Hata mbeleko kukaa, mbali sana katembea,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Ushirika kuzaliwa, afueni wakajua,
Kada wakateuliwa, kuufagia na kuua,
Hadi ilipofikia, Kama mzoga ukawa,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Kahawa ikapotea, kwa beize kupungua,
Chai nayo hiyo pia, tukanywa hadi kulewa,
Mapato yakapungua, na nyumba kuteketea,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Pamba ikahujumiwa, na viwanda kujifia,
Mangimeza watumia, mkulima aumia,
Uongo twasingizia, ukweli tunaujua ?
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Mfumo umedumaa, pande moja kuonea,
Kodi watutamkia, hali mtaji mwatwaa,
Si bure mnaugua, si uzima ni kichaa,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Mwazidi tushindilia, na maisha kuchimbua,
Nini tunategemea, ila kuaga dunia,
Vijiji vinajifia, wazee wamebakia,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Akili zimepagawa, twashindwa vihudumia,
Vijiji pepo Rashia, na leo Japani pia,
Watu wavikimbilia, waogopa nyuklia,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Vijiji vya Tanzania, pepo ingelikuwa,
Wengi tungelihamia, miji tukawaachia,
Akili zetu kukua, miili kupata afya,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Mbaya chama kimoya, shetani aliyekua,
Wenyewe waliamua, wakawa ndio sheria,
Leo tusipokataa, wanaweza kurudia,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Vyama vingi ndiodawa, unyonyaji kukataa,
Ona na wabunge pia, malaki wanachukua,
Masikini tunalia, wao wanafurahia,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Wakulima mashujaa, sio chama kimoya,
Ushindani mwatakiwa, sikuzote kuwania,
Ili kuja kutetewa, haki yenu kuambua,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Kuuza na kununua, pasipo kuingiliwa,
Walanguzi kuwatoa, ukawa ni wenu ubia,
Watu wa nje najua, wapo kuwasaidia,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Hamsini mmevia, mwazidi nyong'onyea,
Naifungua dunia, mpya njooni kukaa,
Ufakiri kukataa, wenyewe mkiamua,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Sababu mnaijua, na uwezo na o pia,
NIa mkidhamiria, muda haitachukua,
Mwingine mnangojea, azuke kuwakomboa?
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Mwingine mnangojea, azuke kuwakomboa?
Mjue hatatokea, si chama wala raia,
Wenyewe mnatakiwa, mapinduzi kuyazaa,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Hivi kweli ayajua, mwana mkulima kua?
Au anajisifia, na dhiki hajaijua,
Ugenini alikaa, au nyumbani kakua?
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Serikali kubwa kua, kwa fujo inatumia,
Kidogo kinachobakia, wengine wanadokoa,
Vijiji kuambulia, haiwezi kutokea,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Huru ingelizaliwa, mikoa ya Tanzania,
Pasi mkuu wa mkoa, waziri mkuu kuwa,
Na bunge la kuamua, yanayofaa mkoa,
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

Unyonyaji ungepungua, na mwisho ukaishia,
Huru kiuchumi kua, mikoa ya Tanzania,
Wakulima wakapaa, na vijiji vikang'aa
Wakulima walinyonywa, wanayonywa, twawanyonya!

No comments: