Wednesday, December 28, 2011

Tanzania italia

Kichekesho kitakuwa, miaka ikitimia,
Watakuja elezea, Makilla alitwambia,
Vingine kumdhania, wala hatukumsikia,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Kaburini nimetiwa, au majivu nishakua,
Wataamka wazawa, na maswali kuyazua,
Wakamaka kuibua, nilikwishawaaambia,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Wajifanyao wajua, nchi wameshikilia,
Kipi kinachoendelea, ila uwizi wakua,
Utume sijaupewa, ila macho nafungua,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Mengi nimeshuhudia, nami nikawambia,
Haifai hii njia, wenzangu kuipitia,
Dhihaka mkajitia, na safari kwendelea,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Na hapa mlipofikia, watu waanza umia,
Kiu kimewazidia na njaa yazidi kua,
Nafuu hawajaijua, umauti walilia,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Na juu waliokua, ukweli hawajajua,
Kama kama watanua, pepo yao ni dunia,
Siku ikiwashtukia, shinikizo kuwaua,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Keki wanatangazia, watu wameshagaiwa,
Hali mkate ruia, hakuna anayeujua,
Hii siyo Tanzania, niliyokwisha kuijua,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Rasilimali zapaa, Ulaya kuelekea,
Wenye mitaa ni njaa, kitu hawakupatiwa,
Madini yachukuliwa, ada kulipa balaa,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Zahanati zimejaa, dawa chini zafukiwa,
Kila mtu analia, roho mbaya tumekua,
Ni nani asiyekuwa, hata wa juu walokua?
Tanzania italia, Makilla aliyasema!

Mshairi ninatua, mbele sintoendelea,
Mzigo niliochukua, hapa chini naachia,
Si mtu wa kuumia, pale pasipo na nia,
Tanzania italia, Makilla aliyasema!


© 2011 Sammy Makilla

No comments: