Wednesday, December 28, 2011

Uchi wanaotembea

Dunia inafichua, uchi wanaotembea,
Wenyewe wanashangaa, wanadhani wamevaa,
Kawaida imekua, ni vigumu kutambua,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

Kitu wasioambiwa, wenyewe wajionea,
Watoto wameshakua, nage wawachezea,
Tikri waikataa, utani wanadhania,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

Ujibari nahofia, hauwezi saidia,
Akili zilotulia, na malengo kuyajua,
Ndicho tunachotakiwa, kuanza kukitumia,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

Huwezi ukatugawa, wazuri na wako wabaya,
Mbali hautofikia, kukwama utatitia,
Kazana macho fungua, ukweli utaujua,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

Uongozi kuachia, vyenyewe hukurudia,
Kitu uking'ang'ania, mwenyewe utaumia,
Haya nimejionea, wana ninavyowalea,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

Ilal ninalolijua, huwa halinayo dawa,
Sikio la kujifia, huwezi kuliokoa,
Wakati ukitimia, lazima kuangamia,
Uchi wanaotembea, wadhani nguo wavaa!

© 2011 Sammy Makilla

No comments: