Monday, December 26, 2011

Yetu hayakuwa yenu

Yetu hayakuwa yenu, panono mlidakia,
Ninasikia fununu, mnautaka ubia,
Cheo mmekichukua, si soda ilobakia?
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

Kwetu haikuwa mbinu, kitabu kilitambua,
Yalitetwa mawazinu, watu hawakusikia,
Viongozi wenye tanu, milango wakaachia,
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

Mchi haujawa kinu, na wala haitakuwa,
Pengine ikiwa tunu, kwa waliokwishajaliwa,
Kwani chao sio chenu, ila chenu hutumia,
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

Mkiwaachia yenu, ukwli wataujua,
Kudharau yao nunu, na watawanyanyapaa,
Muishiwe nazo mbinu, yenu mkayachukia,
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

Wenyewe wanazo menu, mambo yao kwa hatua,
Kuingia ndani mwenu, kisha kuwavurugia,
Mkawa hamna lenu, vyema linaloendelea,
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

Wanatumia upenu, kule mnakoegemea,
Wanunua watu wenu, na siri wanawaambia,
Kuna waitwao Manu, au Imma mtawajua,
Yetu hayakuwa yenu, na wala hayatakuwa.

No comments: